Aliyoyasema Kikwete nyumbani kwa Lowassa

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo katika msiba wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyefariki jijini Dar es Salaam. Msiba wa Lowassa upo nyumbani kwake, Masaki jijini Dar es Salaam.Picha na Sunday George
Muktasari:
- Lowassa aliwahi kueleza yeye na Kikwete hawakukutana barabarani
Dar es Salaam. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amemzungumzia hayati Edward Lowassa akisema walifahamiana na kuzoeana tangu walipokuwa vijana.
Amesema hata Lowassa alipopata changamoto na kukaa pembeni, waliendelea kuwa pamoja na kushirikiana kwenye kila lililowezekana.
Kikwete ameeleza hayo leo Februari 12, 2024, Masaki jijini Dar es Salaam, alikoenda kuhani msiba wa Lowassa.
Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024 saa nane mchana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kikwete amesema walifanya kazi na Lowassa katika Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM), kwenye chama na hata kwenye siasa na Serikali.
"Nilikuwa wa kwanza kuingia kwenye chama, yeye alifuata. Baadaye nilienda jeshini, mwenzangu aliendelea kuwa mbunge, kisha nami nikateuliwa kuwa mbunge," amesema.
Baada ya uteuzi huo, amesema wote wawili waliteuliwa kuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri na walifanya kazi pamoja wakiwa huko.
Ameeleza Lowassa alikuwa na mchango mkubwa kwa Taifa na kwamba, yaliyotokea ni changamoto katika maisha lakini hayafuti mema na mazuri aliyoyafanya.
Februari 7, 2008 kutokana na mjadala wa taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond Development Company LLC ya Huston, Texas, Marekani mwaka 2006, Lowassa alilazimika kujiuzulu uwaziri mkuu.
Hatukukutana barabarani
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 25, 2011 wilayani Monduli mkoani Arusha, Lowassa alisema: “Nitakuwa ni mtu wa mwisho kufikiria au kupanga kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama na Rais ambaye nimemuunga mkono kwa dhati kwa muda mrefu na kushirikiana naye katika harakati nyingi za kifikra na za kiuongozi katika ngazi mbalimbali na kwa miaka mingi. Nilipata kulisema hili na leo nalirudia. Mimi na Rais Kikwete hatukukutana barabarani.”
Lowassa alisema hayo akitoa ufafanuzi kuhusu matukio ambayo yalimhusisha yeye binafsi, akidai kuwa yalikuwa yakitishia ustawi na mshikamano wa kimaadili, kihistoria na kikazi miongoni mwa viongozi na baina ya wanachama wa CCM.
Walivyowania urais
Kikwete pia ameeleza namna walivyoshauriana na Lowassa, kuchukua fomu kugombea urais mwaka 1995.
"Siku moja asubuhi nikapokea ugeni, mtoto akaja chumbani kuniambia baba kuna wageni. Nikawakuta marafiki zangu watatu," amesema.
Amewataja marafiki hao kuwa Samuel Sitta (aliyekuwa Spika wa Bunge), Rostam Azizi na Lowassa.
Amesema Sitta aliwaambia Lowassa na Kikwete waende Dodoma kuchukua fomu kugombea urais.
"Mimi nikasema jambo hilo halikuwepo kwenye mawazo yangu kama mwenzangu, (Lowassa) lipo kwenye mawazo yake mwacheni aende," amesema.
Baada ya kauli yake, amesema Lowassa alisema bila Kikwete hataenda kuchukua fomu, ndipo walipokubaliana wote wakaenda kuchukua fomu.
"Tukachukua fomu tukapitia mchakato wa ndani wa chama (CCM). Mwenzangu hakubahatika. Mimi nilibahatika ndani ya watano, baadaye ndani ya watatu, nikaenda kwenye wawili na hapo kura zangu hazikutosha, Benjamin Mkapa akapata nafasi hiyo," amesema.
Pamoja na mapito hayo, Kikwete amesema waliendelea kuweka mikakati ya pamoja ya mwaka 2005.
"Mwaka 2005 tulikuwa na timu kubwa, nikateuliwa kugombea mwenzangu akawa Waziri Mkuu, akapata changamoto katikati ikabidi akae pembeni, lakini tuliendelea kuwa pamoja na kushirikiana kwenye kila lililowezekana," amesema.
Boys II Men
Katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995 na ule wa 2005 kuliibuka kundi la ‘Boys II Men’ ambalo liliwahusu Kikwete na Lowassa.
Ni nguvu za wawili hao baada ya kukosa nafasi ya kuteuliwa kugombea urais 1995, mwaka 2005 wakakubaliana Kikwete ndiye agombee na Lowassa amuunge mkono.
Maandiko mengi ambayo hayajakanushwa kikamilifu, yanasema wawili hao walikubaliana Kikwete aanze mihula miwili (2005-2015), halafu amsaidie Lowassa kuwa Rais kwa muhula unaofuata yaani uchaguzi wa 2015 na ule wa mwaka 2025.
Haikuwa rahisi kupenya mwaka 1995 kutokana na kizingiti cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye tangu walipochukua fomu za urais wakasafiri pamoja kwa ndege, kwani inaelezwa hakuupenda urafiki wa wawili hao.
CCM ikarejesha majina matatu tu ambayo yalipelekwa kwenye ngazi ya juu ya mchujo, jina la Lowassa halikuwapo kwani tayari Baba wa Taifa ambaye aliheshimika sana, inaelezwa alikuwa ametilia shaka utajiri wake.
Katika mzunguko wa kwanza wa kura za maoni, Kikwete aliibuka mshindi kwa kupata kura 534, akifuatiwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye alikuja kuwa Rais kwa kupata kura 459 na mzee Cleopa Msuya aliyepata kura 336.
Hata hivyo, upigaji kura ulienda mzunguko wa pili kwa maelezo kuwa Kikwete hakupata kura nyingi (simple majority) kati ya kura 1,331 zilizopigwa na wajumbe wa CCM, hivyo mzunguko wa pili, Mkapa akapata 686 na Kikwete 639.
Alivyowasili msibani
Kikwete alifika msibani saa 7.58 mchana akiambatana na mkewe, Salma Kikwete, wasaidizi wake na watu wengine, msafara wake ukiwa na takribani watu 12.
Baada ya kuwasili msibani alipokewa na viongozi wa Serikali waliokuwepo eneo hilo.
Mapokezi yalipokamilika Kikwete alienda moja kwa moja eneo lenye kitabu cha maombolezo, kisha aliingia ndani kuhani wafiwa.
Ilichukua takribani dakika tatu kuwa ndani, baadaye alitoka na kuzungumza na wanahabari. Alipomaliza aliagana na viongozi na waombolezaji wengine kisha akaondoka saa 8.13 mchana.