Anna Mghwira alivyoacha alama Kilimanjaro

Anna Mghwira alivyoacha alama Kilimanjaro

Muktasari:

  • Wako baadhi ya wakuu wa mikoa ambao kuondolewa kwao na Rais Samia Suluhu Hassan katika mikoa waliyokuwa wanahudumu kumepokewa kwa furaha na baadhi ya wananchi, lakini si kwa Anna Mghwira aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Moshi. Wako baadhi ya wakuu wa mikoa ambao kuondolewa kwao na Rais Samia Suluhu Hassan katika mikoa waliyokuwa wanahudumu kumepokewa kwa furaha na baadhi ya wananchi, lakini si kwa Anna Mghwira aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Ndio maana alipoandika ujumbe wa kuwaaga wana Kilimanjaro kupitia ukurasa wake wa Facebook, hakuna mchangiaji aliyetaja la kiongozi huyo, isipokuwa karibu wote walionyesha kuumizwa na jambo hilo.

“Ninamshukuru Mungu kwa muda wote nilioishi na kufanya kazi Kilimanjaro. Asanteni kwa ushirikiano na mshikamano. Tuendeleleze umoja huu na nguvu ya pamoja kwa maslahi ya mkoa na Taifa. Nitawakumbuka Daima…,”aliandika mama Mghwira kwenye ukurasa wake.

Lamtey Edwin aliandika “Mungu akubariki kwa utumishi wako uliotukuka ndani ya mkoa wa Kilimanjaro, daima tutakukumbuka mama yetu.” huku Florah Temba akiandika, “Asante mama umetufundisha umoja, Mungu aendelee kukutunza”.

Lema Emmy alisema “Dahhh basi sawa tuu. Asante mama kwa hekima na akili kubwa uliyoitumia Kilimanjaro. Angalia kila mmoja anasema asante ila kiukweli kila mtu anamani ungebaki walau basi miaka mingine miwili tu”.

Anna Lyimo aliandika katika ukurasa huo, “Tunaomba apewe ubalozi na ni msomi ni Dk Anna Elisha Mghwira. Sema alijishusha sana ili aendane na wananchi wake na kuondoa gap (tofauti) na watumishi wake.”

Kwa upande wake, MC Gasto Gasper aliandika “Mama hongera, ulionyesha mfano mzuri kama kiongozi. Umeishi na watu wote wa Kilimanjaro kama ndugu. Uongozi wako ulikuwa na hekima ya Mungu. Tutakuombea sana”.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alimwelezea mama Mghwira kama kiongozi aliyeimarisha usalama, kushughulikia majanga na aliunganisha wakazi wa mkoa huo bila kujali itikadi, dini au jinsia.

Mbunge wa Moshi mjini (CCM), Priscus Tarimo alisema mama Mghwira alikuwa mchapa kazi, mzalendo, mwanaharakati na atakumbukwa kwa juhudi zake za kutafuta maendeleo ya mkoa huo lakini pia kuifufua benki ya Ushirika Kilimanjaro.