Anusurika kifo kisa Sh1,000

Anusurika kifo kisa Sh1,000

Muktasari:

  • Mgusuhi Sabayi anasakwa na polisi wilayani Serengeti kwa madai ya kumjeruhi,  Silikale Mwita akipinga kutolewa katika sherehe ya harusi kwa kushindwa kulipa Sh1,000 ili aendelee kucheza muziki na wasichana.

Serengeti. Mgusuhi Sabayi anasakwa na polisi wilayani Serengeti kwa madai ya kumjeruhi,  Silikale Mwita akipinga kutolewa katika sherehe ya harusi kwa kushindwa kulipa Sh1,000 ili aendelee kucheza muziki na wasichana.

Tukio hilo lililotokea leo Jumanne Februari 9, 2021 ni la pili ndani ya miezi mitatu kwani Oktoba 31, 2020 Nchagwa Safi mkazi wa kijiji cha Merenga alikamatwa kwa madai ya kumuua  Kegoka Mwikwabe (21) kwa madai ya kumfukuza kwenye harusi asicheze na wasichana  kwa kukosa Sh2000.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo mwenyekiti wa kitongoji cha Nyabirore kijiji cha Kenokwe, Chacha Zablon amesema tukio hilo limetokea saa 10 alfajiri nyumbani kwa Mang'o Kibuni aliyekuwa akimuozesha binti yake.

"Ukumbini huwa na wasichana wengi ambao wanaingia bure, wanaume wanatoa fedha ili waingie kucheza nao, humo ndani baadaye wanaanzisha mtindo wa kutoana kwa fedha kama njia ya kujiongezea kipato bibi harusi na vijana kujionyesha kwa wasichana maana hiyo ni fursa ya kupata wachumba.”

" Sabai alitolewa kwa Sh500 ili kama ana Sh1000 abaki akataka kukaidi wakamtoa akawa amekasirika akitaka  Silikale naye  atoke kwa kuwa hakutoa fedha. Mzozo  baada ya kupamba moto aliyejeruhiwa alitoka nje kumfuata mtuhumiwa ambaye alimchoma kisu tumboni,” amesema.

Naye Kibuni amesema, “nilipotoka nje nilimkuta amelala chini damu zinavuja sana, watu wote wakawa wametawanyika na muziki ukazimwa. Nilimtaarifu mwenyekiti wa kitongoji akaja na kumkimbiza majeruhi hospitali huku mtuhumiwa akiwa ametoroka.”

Mganga mkuu wa hospitali ya Nyerere, Tanu Warioba amekiri kumpokea majeruhi na kwamba anaendelea na matibabu huku mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu akisema polisi wanaendelea kumsaka mtuhumiwa.