Arusha wapigwa ‘stop’ kufyatua fataki mwaka mpya bila kibali

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo
Muktasari:
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limepiga marufuku kufyatua fataki bila kuwa na kibali na kuchoma matairi barabarani katika mkesha wa kusherehekea Mwaka Mpya 2022.
Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha limepiga marufuku kufyatua fataki bila kuwa na kibali na kuchoma matairi barabarani katika mkesha wa kusherehekea Mwaka Mpya 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Desemba 29, 2021 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Justine Masejo amesema polisi wamendaa doria za miguu na magari kudhibiti uhalifu katika Jiji la Arusha.
Amesema ulinzi utaimarishwa katika nyumba za ibada na maeneo mbalimbali ili kuhakikisha watu wanasherehekea vizuri mkesha wa Mwaka Mpya 2022.
Kamanda amesema katika maadhimisho ya mwaka mpya ni marufuku kupeleka watoto wadogo katika kumbi za starehe.
"Katika maadhimisho haya pia tunawaomba wenye baa kufuata maagizo ya leseni zao kwa kufanya biashara kuzingatia sheria"amesema
Kamanda Masejo pia amewataka Wananchi kuchukuwa tahadhari Kwa kufunga Nyumba zao wanapokwenda katika mkesha wa mwaka mpya.