Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Asilimia 79 kidato cha nne 2022 waanguka hisabati

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) likitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022, somo la hisabati limeendelea kuwa kitendawili kisichoteguka baada ya asilimia 79.92 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo kufeli.

Mtihani huo uliofanyika kati ya Novemba 14 hadi Desemba mosi mwaka jana uliwahusisha watahiniwa 566,636 lakini 415,844 sawa na asilimia 79.92 walifeli hisabati kwa kupata alama F. Hata hivyo, ufaulu huo mdogo umeimarika kidogo ikilinganishwa na mwaka juzi ambao asilimia 80.46 walifeli kwa kiwango hicho.

Hata hivyo, wadau wa somo hilo wamesema umefika wakati sasa ifanyike tathmini itakayoonyesha tatizo lilipo na hatua stahiki zichukuliwe.

Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi alisema waliopata alama D katika somo hilo ni wanafunzi 48,476 sawa na asilimia 9.32.

“Wanafunzi 34,783 sawa na asilimia 6.68 wamepata daraja C, wengine 9,984 sawa na asilimia 1.92 wamepata B na 11,245 sawa na asilimia 2.16 wamepata A,” alisema Amasi.

Hakuna somo jingine ambalo waliopata alama F wamefikia au kuzidi asilimia 50, kulingana na taarifa ya matokeo hayo ikilinganishwa na mwaka juzi ambapo asilimia 51 walifeli somo la uraia.

Kutokana na ugumu wa somo la hisabati, Mhadhiri wa Hesabu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Said Sima alisema inahitajika kufanywa tathmini kujua mzizi wa tatizo.

Iwapo utajulikana, alisema mara moja uanze utaratibu wa kupanga namna ya kulitatua kwa kuchukua hatua zinazotakiwa.

“Limekuwa tatizo la muda mrefu hivyo linahitaji lishughulikiwe kulingana na mazingira ya Tanzania. Katika miaka ya 1970 ufaulu ulikuwa hadi zaidi ya asilimia 50 tofauti na kinachotokea sasa, tufanye tathmini kujua shida iko wapi,” alishauri Dk Sima.

Maoni ya mhadhiri huyo hayatofautiani sana na Dk Sylvester Rugeiyamu wa UDSM aliyesema uwiano mdogo wa walimu wa hisabati na wanafunzi ni miongoni mwa sababu za anguko.

“Ukilinganisha walimu wa masomo mengine na somo la hisabati kuna tofauti kubwa, Serikali inaona tatizo na lipo muda mrefu itafute namna ya kulitatua,” alisema.

Kuhusu ufaulu wa ujumla, kaimu mtendaji huyo wa Necta alisema katika watahiniwa wote waliofanya mtihani, 456,975 sawa na asilimia 87.79 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne wakiwamo wavulana 243,285 sawa na asilimia 87.08 na wasichana ni 213,690 sawa na asilimia 88.60.

Kwa msingi huo, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.49 kutoka watahiniwa 422,388 waliofaulu mwaka juzi.

Wakati hali ikiwa hivyo, Amasi alisema wanafunzi 333 wamefutiwa matokeo baada ya kubainika kufanya udanganyifu na kati yao mmoja ni mwanafunzi wa maarifa (QT).

Mbali na wanafunzi hao, alisema wengine watatu wamefutiwa matokeo kwa kuandika matusi katika majibu ya mitihani yao huku vituo vitatu vya mtihani vikifungiwa.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Andrew Faza Memorial chenye namba ya usajili S2365) na Cornelius (S0265) vya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Mnemonic Academy (S5387) cha Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

Shule ya Andrew Faza ilikuwa na watahiniwa sita, Cornelius watahiniwa 21 na Mnemonic walikuwa 27 wa kujitegemea ambao wote wamefutiwa matokeo.

Alipoulizwa kuhusu hatua dhidi ya wanaojihusisha na udanganyifu, alisema wanaofutiwa matokeo taarifa zao hupelekwa katika mamlaka za ajira zao na kwingineko kunakoshughulika na kesi za jinai ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Kama ilivyokuwa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana, haya pia hakukuwa na mpangilio wa shule, wanafunzi na mikoa 10 bora iliyoongoza kitaifa.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Amasi alijibu baraza limetathmini na kutoona tija ya uwepo wake hivyo watu waache mazoea.

“Ina tija gani kumtaja mmoja kati ya shule nyingi na tena bahati mbaya unamlinganisha na mwingine ambaye hawakusoma kwenye mazingira yanayofanana,” alisema.

Alifananisha kitendo cha kupanga orodha ya shule 10 bora zilizofaulisha zaidi ni sawa na kuzitangazia soko kwa wazazi ili wawapeleke watoto wao huko badala ya ushindani.

“Kutangaza shule ya kwanza huenda tunaifanyia marketing, kwa hiyo jambo ambalo halina tija tumeona tuondokane nalo.

“Ina tija gani kumtaja mmoja kati ya shule nyingi na tena bahati mbaya unamlinganisha mtu na mwingine ambaye hawakusoma kwenye mazingira yanayofanana?” alihoji Amasi.