Asilimia 83 majeruhi ajali barabarani hupoteza nguvu kufanya kazi

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya dharura Muhimbili, Dk Biita Muhanuzi
Muktasari:
Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha dharura kimesema asilimia 83 ya majeruhi wa ajali za barabarani wanaopokelewa katika kitengo hicho, upona lakini upoteza nguvu ya kufanya kazi na kuzalisha.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha dharura kimesema asilimia 83 ya majeruhi wa ajali za barabarani wanaopokelewa katika kitengo hicho, upona lakini upoteza nguvu ya kufanya kazi na kuzalisha.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura Muhimbili Dk Biita Muhanuzi wakati wa semina ya siku mbili ya waandishi wa habari juu ya usalama barabarani iliyoandaliwa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA).
Amesema asilimia hizo ni kwa mujibu wa takwimu za kitengo hicho na kubainisha kuwa wengi wa majeruhi wa ajali wanaofika ni wanaume ambao ni asilimia 75 huku wanawake wakiwa asilimia 24.
“Umri wa majeruhi hawa tunaowapokea ni kuanzia miaka mitano hadi 28, hawa sio wazee bali ni nguvu kazi ya taifa na wanatakiwa kuzalisha lakini uishia kulazwa na hata wakipona upoteza uwezo wa kufanya kazi,” amesema
Aidha amesema vifo vinavyotokana na ajali hapa nchini ni vingi kuliko vile vinavyotokana na HIV, TB na Maralia hivyo ni muhimu kuzuia ajali hizo zisitokee ili kuepusha vifo.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani, ASP Musa Manyama amesema kwa mujibu wa takwimu za jeshi la polisi ajali za barabarani zimepungua nchini kutoka 978 mwezi Januari hadi Juni mwaka 2020 hadi kufikia 760 kwa kipindi kama hicho mwaka huu.
“Pamoja na juhudi zinazofanywa na jeshi la polisi, zinahitajika jitihada za pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuweza kupambana na tatizo hili la ajali hapa nchini, tukumbuke kwamba ajali hazitokei bali zinasababishwa na watu,” amesema
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Idara Tafiti za Sheria kutoka Umoja wa Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), Augustus Fungo amesema muongo wa hatua za kuimarisha usalama barabarani ni matokeo ya juhudi zinazofanywa na Umoja wa Mataifa kutoa suluhisho la tatizo la usalama barabarani duniani.
Amesema muongo huo ambao ni wa kwanza ulitangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi 2010, kwa kipindi cha 2011-2020 una lengo la kuokoa mamilioni ya maisha ya watu yanayopotea barabarani kila mwaka.