Prime
Asimulia namna fisi alivyomletea ulemavu
Rose Kapande, mkazi wa Kijiji cha Espai akizungumza na mwandishi wa Mwananchi. Picha na Janeth Joseph
Ngorongoro. Msemo kwamba hujafa hujaumbika, unaweza kufaa kuelezea masaibu yaliyomkuta Rose Kapande (50), mkazi wa Kijiji cha Esapai, Wilaya ya Ngorongoro baada ya kupoteza mikono na kujeruhiwa sehemu ya uso kwa kung’atwa na fisi.
Mwanamke huyo ambaye anaishi katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro alijeruhiwa mwaka 2018 wakati akimfukuza fisi aliyeingia kwenye boma lake la ng’ombe na mbuzi akitaka kula mifugo yake.
Mwanamke huyo ambaye ni mama wa watoto tisa, anaeleza kuwa wakati tukio hilo saa nane usiku, alikuwa peke yake baada ya kuachana na na mume wake.
Anaeleza kuwa wakati amelala ndani alisikia kitu kinagongagonga kwenye boma la ng’ombe na akatoka nje kuona ni kitu gani.
Alipofungua mlango, anasema alimuona fisi akipambana na mifugo yake na akaanza kumfukuza fisi yule ili asile mifugo yake.
Wakati akimfukuza fisi huyo alimgeukia na kuanza kumshambulia yeye sehemu za mikono, kichwa na eneo la uso ambapo aliliwa jicho moja la kulia.
“Nikiwa nimelala fisi alikuja nyumbani saa nane usiku, akawa ameingia kwenye boma la ng’ombe na mbuzi. Sasa nikiwa niko ndani nikasikia nje kama kuna kitu hakipo sawa, baada ya kusikia kitu kinagongagonga boma la ng’ombe na mbuzi nikawa nimefungua mlango kutoka nje,” anasema Rose katika mahojiano na gazeti hili.
“Wakati natoka nje nikamwona fisi, nikawa namtishia ili aondoke, yule fisi akanigeukia akaanza kupambana na mimi. Aliniuma na kunichanachana sehemu ya kichwa na sehemu ya uso upande wa kulia, alinitoa hadi jicho.
“Kwa hiyo upande mmoja wote uliharibika na mikono yote aliitafuna,” anasimulia
“Baada ya kunijeruhi alirudi tena kwenye boma la ng’ombe na kuijeruhi tena mifugo iliyokuwepo ndani, baada ya kuniachia nikiwa na majeraha makali. Nilipiga ukunga, bahati nzuri majirani zangu walikuja kunisaidia ambapo walinichukua na kunipeleka hospitali ya KKKT, hapa Karatu.
“Baadaye nilipelekwa Hospitali ya Mount Meru ambayo iko Arusha na baadaye hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC kwa matibabu makubwa zaidi,” anasema
Maisha yake kwa sasa
Rose anasema kwa sasa maisha yake ni magumu kwa kuwa hana mikono na upande mmoja wa kichwa na sehemu ya uso vyote viliharibiwa na fisi na hivyo hawezi kufanya shughuli yoyote ya kumuingizia kipato.
“Sasa hivi mimi ni mlemavu, sina mikono na upande wangu mmoja wa kichwa na uso ni mbovu, nipo tu hapa nasaidiwa na wasamaria wema, maana watoto wangu wote walishaolewa, kwa hiyo chakula nalishwa kama mtoto mdogo, nguo navalishwa yaani sijiwezi chochote hapa nilipo,” anaeleza.
“Naishukuru Serikali nimepona mpaka kwa namna ambavyo walinipigania kuokoa maisha yangu, nimebaki mlemavu na hali yangu ya maisha ni ngumu, mpaka sasa kutokana na maisha niliyopitia naishi kwa hofu hapa nilipo kutokana na wanyama wakali walipo katika hifadhi hii,” anasema.
Ombi lake kwa Serikali
Kwa kuwa amekuwa akiishi kwa hofu kijijini hapo ameiomba Serikali imsaidie aondoke katika hifadhi hiyo imtafutie sehemu nyingine ya kwenda kuishi kama ambavyo watu wanavyohamishwa kwa sasa.
“Mimi niliomba kuondoka hata kabla hii shughuli ya kuwaondoa watu halijaanza, naomba Serikali inisaidie niende kuishi sehemu salama zaidi, nitafurahi sana maana najua nitakwenda kuishi sehemu salama nikitoka huku hifadhini maana maisha yangu tangu kipindi hicho yamekuwa na hofu kubwa sana tangu nijeruhiwe,” anasema
Pamoja na mambo mengine ameiomba Serikali impe msaada kwani hapo alipo ni mlemavu na hakuna chochote ambacho anaweza kufanya cha kumpa rizki.
Anaongeza, “mimi ni miongoni mwa watu ambao walioenda kutembelea Msomera maisha ya kule nayaona ni mazuri yatanifaa zaidi na nitakuwa nimesaidiwa sana na Serikali, naiomba Serikali iharakishe kukamilisha mpango wa sisi kwenda kule Msomera maana naona kama vile nacheleweshwa kuondoka, tunaelendelea kuishi katika mazingira hatari huku hifadhini na wanyama.”
Mmoja wa majirani aliyefika wakati mama huyo anavamiwa na fisi, Petro Kashuu anasema maisha ya watu katika eneo hilo ni magumu kutokana kwa kuna wanyama wengi kama fisi na watu wamekuwa wakiishi kwa hofu.
“Huyu mama wakati alipojeruhiwa na fisi tulikuwepo, na hili eneo limekuwa na fisi wengi, tumekuwa tukiteswa na wanyama hapa kijijini. Maisha ya huku ni hatari kwa sababu wanyama wamekuwa wakitujeruhi licha ya kwamba huku watu wamezoea kuishi na wanyama.
Ilichokisema Ngorongoro
Naibu Kamishna Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Elibariki Bajuta alisema baada ya tukio hilo kutokea, Serikali ilifanya jitihada za haraka kuokoa maisha ya mwanamke huyo kwa kuhakikisha anapata matibabu yanayostahili.
“Ni kweli tunafahamu tukio hili la huyu mama kujeruhiwa na fisi na viungo vyake kuliwa. Huyu mama alikwenda kuokoa mifugo yake baada ya kusikia fisi ameingia kwenye boma la ng’ombe hivyo wakati anapambana kuokoa mifugo yake alivamiwa na fisi,” alisema
“Fisi walitafuna viganja vyake vya mikono na sehemu kubwa ya uso na upande wa kulia wa kichwa chake na kumuathiri upande wa kulia wa fuvu na sehemu ya mdomo,” alisema Bajuta.
“Mamlaka kwa kuwa tuna kituo cha ulinzi na timu za uokoaji baada ya kupata taarifa hizi vijana wetu kwa kushirikiana na majirani tumlimsaidia kuhakikiasha anapata huduma stahiki,” alisema.
Aidha alisema matukio ya watu kuathiriwa na kuvamiwa na wanyama wakali katika hifadhi hiyo ni mengi yakihusisha wanyama kama vile chui, fisi, simba na tembo .
“Sisi kama Mamlaka tunaendelea kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari lakini mnyama ni mnyama tu hazoeleki.
“Tunafurahi mama huyu kwa sasa anataka kuhama hifadhini kwenda sehemu anayotaka na suala hili la watu kutakiwa kuhama kwa hiari ni kwa ajili ya usalama wa maisha yao na uhifadhi,” alisema.