Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askari polisi matatani akidaiwa kumvunja mguu mtuhumiwa kituoni

Peter Charles anaedai kavunjwa mguu na askari polisi

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amesema uchunguzi umeanza na hatua za kisheria zitachukuliwa endapo atabainika kuwa na hatia.

Arusha. Ofisa Upelelezi Wilaya ya Arusha Mjini, Omary Mahita ameingia matatani kwa tuhuma za kumpiga hadi kumvunja mguu mtuhumiwa wakati wa mahojiano akiwa kituo cha polisi.

Askari huyo anatuhumiwa kumvunja mguu wa kushoto Peter Charles (21), mkazi wa Daraja II, jijini Arusha Juni 6, 2024. 

Akizungumzia tukio hilo leo Alhamisi Agosti 15, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema uchunguzi umeshaanza na endapo atabainika kuwa na kosa, atachukuliwa hatua za kisheria.

"Ni kweli hilo tukio liko ofisini kwangu na tumeanza uchunguzi tangu Agosti 8, 2024 nilipopata taarifa kwa simu kutoka kwa ndugu wa huyo kijana akimtuhumu askari wangu kumpiga hadi kumvunja mguu,” amesema Masejo alipozungumza na Mwananchi.

Amesema alimuita mlalamikaji na kumkutanisha na mtuhumiwa, akamtambua na akatoa malalamiko ndipo akafungua jalada.

Hata hivyo, amesema upelelezi unaendelea, huku akisisitiza hakuna mtu aliye juu ya sheria.

“Upelelezi ukikamilika tutamchukulia hatua askari huyo endapo itabainika alitenda kosa hilo kwa kujichukulia sheria mkononi hadi kujeruhi,” amesema Kamanda Masejo.


Asimulia ilivyokuwa

Akisimulia mkasa mzima, kijana Peter amedai Mei 29, 2024, saa 1:20 usiku akiwa nyumbani kwa mmoja wa marafiki zake eneo la Daraja II wakitazama sinema kwenye luninga, walifika askari watatu kati yao mmoja alikuwa dereva.

Amedai waligonga mlango na kujitambulisha, kisha wakawataka watoke nje na walipotoka wakawaambia waingie kwenye gari walilokuja nalo askari hao.

“Walituchukua hadi kituo cha Polisi Kati bila kutuambia kosa letu, tulipouliza walituambia tutajua huko huko kituoni,” amedai kijana huyo.

Amedai walikaa kituoni siku tatu bila kuelezwa chochote na siku ya nne waliitwa katika chumba cha mahojiano na kuhojiwa kwa nini wanacheza kamari mitaani.

“Tulikataa kuwa hatuchezi kamari, lakini hawakutaka kutuamini zaidi ya kutupiga kwa marungu kwenye magoti, mgongoni na kiunoni wakidai kukubali kwetu ndio msamaha wetu. Hata hivyo tuliendelea kukataa na kurudishwa rumande tukiwa na maumivu makali,” ameeleza kijana huyo.

Amedai ilipofika siku ya saba, waliitwa tena wakanza kushushiwa kipigo na askari wawili, huku akimtaja mmoja kuwa alisikia wenzake wakimuita kwa jina la Mahita.

Baada ya kipigo, aliwaamuru kulala kwa tumbo na akaanza kuwakanyaga miguu.

“Alipofika kwangu alinikanyaga kwa nguvu mpaka mfupa wa mguu ukavunjika na ulitoa mlio mithili ya kuni iliyovunjwa na damu zikaanza kutoka mfululizo,” amedai Peter.

Amedai alipobaini amemvunja mguu, askari huyo akawaambia wanyanyuke na kuuliza hizo damu za nani, “nikamjibu ni zangu, lakini wenzangu nao walikuwa na michubuko akaturuhusu tukanawe bombani turudi mahabusu,” amedai Peter.

Amesema kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo, alipiga kelele usiku mzima na ilipofika asubuhi askari mmoja aliingi mahabusu alipomuona alikwenda kumchukulia dawa za kutuliza maumivu anywe.

“Hata hivyo sikupata nafuu, walileta chumvi nyingi na kunimwagia kwenye kidonda changu wakaondoka,” amedai Peter.

Pater amedai Juni 5, 2024 waliletwa vijana wengine wanne mahabusu, kabla ya kesho yake siku ya tisa kuitwa kwa pamoja chumba cha mahojiano na kusomewa shtaka linalowakabili wote saba la wizi wa kutumia silaha na wakarudishwa mahabusu wakawa wanasubiri kukamilika kwa maandalizi ya jalada ili wapelekwe mahakamani.

 “Tulibaki tunashangaa, inakuwaje tunageuziwa shtaka, mara akaja yule askari Mahita akatuambia kwa sababu tumekataa kosa la kamari, tutakwenda jela kupambana na kesi ya wizi wa kutumia silaha,” amedai Peter.

Mjomba wa Peter, aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema waligundua kijana wao amekatwa baada ya siku tatu, walipofuatilia polisi kwa lengo la kumuwekea dhamana walinyimwa.

Amesema waliamua kupiga simu Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) na wakatakiwa watume RB namba kabla ya kuambiwa dhamana iko wazi siku hiyohiyo.

“Ijumaa nikarudi kituoni kumdhamini mpwa wangu, lakini nikaambiwa nirudi Jumatatu atapelekwa mahakamani kwa sababu kosa lake halidhaminiki kwa sababu RB namba ilikosewa kuandikwa kosa la kamari, ila kosa lake ni wizi wa kutumia silaha,” amedai mjomba huyo.

Amesema aliomba angalau amuone ndugu yake, lakini alikataliwa ikabidi asubiri hadi Jumatatu waliyosema ndipo akapewa dhamana.

Amesema Peter alikuwa ameumia, aliwaomba wampatie PF3 akatibiwe, lakini walimgomea.

“Ilibidi nikadanganye Kituo cha Afya Olorien kuwa ameanguka wakampokea wakamsafisha vidonda na wakampiga X-Ray ikaonyesha amevunjika vibaya, nikatakiwa kwenda Hospitali ya Seliani.”

“Kwa kuwa daktari alisisitiza niende na PF3, kesho yake ilibidi twende Kituo cha Polisi Kijenge nako tukadanganya ameumizwa na rafiki yake nikapewa na nikaambiwa nirudi tena kwa ajili ya kufungua jalada,” amesimulia mjomba huyo.

Hata hivyo, mjomba huyo amesema kwa sasa wanasubiri majibu ya upelelezi unaofanywa na Jeshi la Polisi kuhusu sakata hilo.