Askari wa JWTZ adaiwa kuua kwa kipigo

Muktasari:
Tatizo la watu kujichukulia sheria mkononi limeendelea kujitokeza baada ya mtu mmoja kuuawa kwa kipigo.
Dar es Salaam. Mkazi wa Kijiji cha Gumba kata ya Gwata Wilayani Kibaha mkoani Pwani, Bakari Mbagara (63) amefariki dunia kwa kile kilichodaiwa kupigwa na waya wa umeme na kulazimishwa kula saruji na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Koplo Chibumba Lugola wa Kikosi cha 121 FIR Ngerengere.
Mbagara alifariki dunia Januari 2 na kuzikwa Januari 3 mwaka huu, katika makaburi yaliyopo kijijini cha Gumba.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,Wankyo Nyigesa alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akisema wanaendelea kumshikilia mtuhumiwa Lugola anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo.
Kamanda Nyigesa alidai kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi walioufanya, inadaiwa Januari 2, askari huyo alimfuata Mbagara kwenye kilabu cha pombe akamchukua na kwenda naye hadi eneo analofanyia biashara akimtuhumu kuwa kamuibia kuku wake.
“Mtuhumiwa alituambia marehemu Mbagara alikuwa anamuibia kuku mara kwa mara, hivyo aliamua kumpiga na kipigo hicho kilimsababishia kifo chake,” alidai
Kifo chake
Akizungumzia kifo cha baba yake, mtoto wa marehemu, Sahau Bakari alisema mtuhumiwa baada ya kumpiga sana Mbagara, alimwachia na kumuamuru aondoke pale na wakati anarudi nyumbani alianguka njiani.
“Wasamaria wema walimchukua na kumkimbiza Zahanati ya Gumba lakini alikuwa ameshafariki na uchunguzi uliofanywa na daktari alituambia kifo chake kimesababishwa na kipigo,” alidai Bakari. Mtoto mwingine wa marehemu, Dunia Said alisema alipigiwa simu na mtuhumiwa kuwa baba yake amekamatwa kwa wizi wa kuku.