Askofu ataja siri nyuma ya kusifia viongozi, ataka wahusika washtuke

Waumini wa kanisa la kiinjili la kiluther (KKKT) Usharika wa Azani Front wakiimba baada ya ibada kumalizika wakati wa sikuku ya krismasi iliyofanyika,jijini Dar es Salaam jana.Picha na Sunday George
Muktasari:
- Awataka viongozi wanaoteuliwa kuwa makini nao kwa kuwa wanaficha udhaifu.
Dar/Mikoani. Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo wametoa ujumbe wa Krismasi kwa waumini wao, ukiwemo unaowataka viongozi wa Serikali kuwa makini na sifa wanazopewa na wateule wao kwa kuwa ni mbinu ya kuficha udhaifu.
Vilevile, wamewataka viongozi pamoja na watendaji watumie sikukuu hiyo kujitathmini kama wanatosha katika nafasi zao.
Viongozi hao wametoa ujumbe huo katika ibada na misa za Krismasi katika makanisa tofauti nchini ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mkombozi wao, Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.
Mafundisho ya viongozi wa dini yamewagusa pia waumini wao wakiwataka kuzingatia mafundisho na kutumia sikukuu ya Krismasi kutafakari maisha yao na uhusiano wao na Mungu.
Wakati viongozi wa dini wakieleza hayo, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu zake za Krismasi na mwaka mpya kupitia ukurasa wake wa Twitter akihimiza wananchi kusherehekea kwa amani, upendo na kiasi, sambamba na kufanya kazi kwa weledi.
Wakati huohuo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye alishiriki misa ya Krismasi katika Parokia ya Kristu Mfalme mkoani Dodoma, aliwasihi waumini na Watanzania kwa ujumla kutoa heshima ya pekee kwa watoto kwa kuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu.
Dk Mpango alisema hivi sasa yanasikika mambo ya hovyo na dhuluma dhidi ya watoto ikiwemo kuwanyanyaswa, kuwaua na kuwalawiti.
“Tumuombe Mungu msamaha na atujalie neema ya kutambua jinsi yeye alivyowapenda watoto na sisi tufanye mengi ya kuwatunza na kumrudishia Mungu wakiwa weupe kama tunavyoweka ishara ya kitambaa cheupe kumrudishia Mungu,” alisema.
Kusifia viongozi
Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Augustine Shao aliwatahadharisha viongozi wakuu wa nchi kuwa makini na sifa wanazopewa na wateule wao akisema “ni mbinu ya kuficha maovu yao”.
Askofu Shao aliwataka viongozi wa kitaifa wasiendekeze sifa hizo akisema hata Mungu alikuwa na madaraka yote lakini hakuyatumia kwa faida yake.
“Tunawaasa viongozi wetu wakuu wa nchi wawe makini na waliowateua, wajue wengi wanaowasifia marais kila waendapo ni mbinu ya kuficha uovu wao wasikubali hili,” alieleza askofu huyo.
Suala la kusifia viongozi limezidi kupata sauti, baada ya Novemba 28 mwaka huu Rais Samia kulizungumzia wakati akifungua mkutano mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), jijini Dodoma alipokosoa bango la kumsifia yeye badala ya sifa hizo kwenda kwa Serikali yake.
Rais Samia alisema amepitia kidogo mambo yaliyotekelezwa ndani ya miaka mitano na kuona kaulimbiu ya mwaka huu inayosema ‘UWT Simama na Samia kwa maendeleo ya Taifa’ inahitaji maboresho.
“Ningependa nifanye marekebisho kidogo, najua hii ndio kauli mliyokuja nayo lakini ingesomeka “UWT simama na Serikali kwa maendeleo ya Taifa,” alisema Rais Samia.Hatua kali zichukuliwe
Aidha, alisema amani ya kweli itakuwepo endapo kila mmoja atawajibika kwa dhati kuheshimu na kulinda viumbe ambavyo ni zawadi ya Mungu.
Huku akikumbushia familia 12 za vigogo ambao wamechepusha maji kwenye bwawa la kuzalisha umeme, askofu huyo alisema kitendo hicho kinastaajibisha.
Desemba 21, mwaka huu mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile katika kongamano la utunzaji mazingira lililofanyika mkoani Iringa alibainisha kuna familia 12 zinazojinufaisha kupitia uchepushaji maji, zikiwemo familia za viongozi wa Serikali na wastaafu.
Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo, aliagiza kushughulikiwa kwa watu waliovamia na kuchepusha maji Bonde la Ihefu.
Askofu Shao alitoa kauli hiyo kupitia waraka wake kwa waumini wa kanisa hilo uliosomwa jana katika misa ya Krimasi Zanzibar.
“Ndugu zangu kiongozi anayejali masilahi ya familia yake huyu ni mbinafsi na hatufai, viongozi hawa ni watu wenye mishahara mikubwa na ya kutosheleza mahitaji lakini kwa sababu ya ubinafsi na uroho wa mali wamefanya wengi kuishi katika hali ya shida kubwa ili wao wafaidi.
“Kutakuwa na amani kama sote tutatenda haki ya kweli na kusikia kilio cha wengi,” alisema Askofu Shao huku akinukuu kitabu cha Yeremia 22: 16-17.
Alisema: “Tunaomba mamlaka ziwachukulie hatua kali na kuwawajibisha. Agizo la Naibu Waziri kwamba waondoke mara moja ni jepesi mno ikilinganishwa na madhara yaliyofanyika.
“Tunasikia pia kwa ajili ya kulindana naibu waziri fulani aliagiza mifugo iliyokamatwa kwa sababu ya uharibifu wa mazingira kwenye bonde waachiliwe mara moja. Kwa akili za Watanzania waliositisha shughuli zao za kujipatia kipato kwa sababu ya kukosa nishati hawawezi kuelewa uwajibakaji wa naibu waziri huyu.
Viongozi wajitathmini
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani aliwaomba viongozi wa Serikali kutumia sikukuu ya Krismasi kujitathmini kama wanatosha katika nafasi zao.
Wito huo umetolewa kipindi ambacho Rais Samia ameshatoa ahadi kakika mkutano mkuu wa CCM Desemba 8, kuwa anakwenda kuunda Serikali na kuwaondoa wale ambao hawaendi na kasi yake.
Dk Chilongani ambaye ni askofu mkuu msaidizi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, alisema:
“Kama unajiona upo kwenye njia iendayo kwa Herode ambayo inaleta mauti, badilisha mwelekeo, rushwa bado inatawala, ufisadi unaongezeka, haki bado inapotoshwa na unyanyasaji bado unaendelea,” alisema.
Askofu huyo alisema anatambua nia ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni njema na anataka watu wapite njia iliyo salama ili wafike Bethelehem lakini chini kuna akina Herode wanaolinda vyeo vyao kuliko kuwatumikia wananchi.
Herode alikuwa mtawala wa Kiyahudi nyakati Yesu anazaliwa, aliyetoa amri watoto wote wa kiume wauawe akihofu kuwa watakuja kupoka madaraka yake.
Mbali na hilo, akihubiri jana katika ibada ya Krismasi, Askofu Chilongani alihoji sababu za Serikali kuwa kimya pindi yanapotokea matukio ya wananchi kuonewa na hata kuuawa.
Alitolewa mfano tukio la hivi karibuni katika Kijiji cha Mwitikila wilaya ya Bahi, kulipotokea mauajia huku viongozi wa kijiji wakitajwa kuwa chanzo.
Wiki mbili zilizopita, gazeti hili liliripoti kifo cha mtu mmoja na wengine kujeruhiwa huku nyumba na mali zikiungua katika kijiji cha Mwitikila chanzo kikiwa ni sungusungu waliodaiwa kutumwa na viongozi wa kijiji.
“Naambiwa mwanakwaya wetu mmoja alirudishwa kijijini huku anatapika damu, mama mmoja alivuliwa nguo akabaki uchi wa mnyama mbele ya halaiki, kwa tuhuma za uchawi, alipigwa viboko na kurushwa kichura hadi akafia porini,” alisema askofu huyo.
Alisema ukimya wa namna hiyo ndio unasababisha wananchi kuchukua sheria mkononi kama walivyofanya wananchi wa Mwitikira walipotoka porini kuchukua mwili wa mama aliyeuawa kwani walichoma gari, duka na nyumba za kiongozi aliyesimamia utesaji na mauji hayo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, ukatili huo hawakuwahi kuuona hata wakati wa utawala wa Wajerumani huku akitaja ukimya wa tukio wa kifo cha Askofu mstaafu, Boniface Kwangu wa Dayosisi ya Victoria Nyanza ambaye mwili wake uliokotwa majini na sasa hawajui kinachoendelea.
Haki, amani vyatawala
Katika hatua nyingine, wito wa haki, amani na upendo kwa wote ulitawala mahubiri na mafundisho ya viongozi hao wa dini katika maeneo mbalimbali juzi wakati wa ibada za mkesha na sikukuu ya Krismasi na jana asubuhi.
Katika kanda ya Ziwa, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu aliwataka waumini na Watanzania wote kudumisha amani na upendo miongoni mwao kama njia ya kudhibiti vitendo vya kihalifu ikiwemo mauaji, mifarakano, vita na ukatili wa kijinsia, hasa dhidi ya wanawake na watoto.
“Dunia imepungukiwa na amani kwa sababu watu hawana mapenzi ya Kristo wala hofu ya Mungu mioyoni mwao, kila kukicha tunashuhudia matukio ya ajabu ikiwemo ya watu kuuana. Kila mtu kwa imani yake amrejee Mungu kwa kuishi maisha ya utakatifu na kutendeana haki kati ya mtu kwa mtu,” alisema Askofu Sangu.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Philadelfia Miracle Temple la Shinyanga, Baraka Laizer aliwataka waumini na wananchi wote kumrudia Mungu hasa pale wanapokumbwa na magumu badala ya kuchukua uamuzi wenye madhara kwa maisha na uhai wa mwanadamu.
Vilevile, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), Zephania Ntunza aliwataka Watanzania kuishi kwa kuvumiliana tofauti zao na kutumia njia ya majadiliano na miafaka kumaliza tofauti zinazojitokeza miongoni mwao.
Askofu Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora naye alilisitiza umuhimu wa kila mmoja kutenda haki kwa mwingine ili kujenga jamii ya watu wanaoishi kwa upendo bila kujali tofauti miongoni mwao.
Akizungumza katika Kanisa ka Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu mjini Tabora usiku wa kuamkia jana, Askofu Ruzoka alisema haki kwa wote, amani upendo ndio ujumbe na mafundisho ya Yesu Kristo unaotakiwa kulindwa.
Ulevi Krismasi nao
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo amewaonya vijana kuacha kunywa pombe kali wakidhani ndiyo maisha ya kisasa huku akisisitiza kwamba vilevi vyenye zaidi ya asilimia 40 ni hatari wa afya zao.
Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, alitoa rai hiyo jana katika usharika wa Moshi Mjini, wakati akihubiri kwenye ibada ya Krismas.
Alisema mtindo wa sasa wa vijana kunywa pombe kali zenye viwango vya vilevi zaidi ya asilimia 40 ni hatari kwa afya zao.
“Naomba nizungumze na vijana, kumetokea mtindo wa vijana wachanga, wenye umri mdogo, kunywa pombe kali sana na wanafikiria eti huo ndiyo mtindo. Kama unataka kuonekana wa kisasa, pombe kali hizi ni hatari, kweli vijana nawaonya, nimeona kuna wimbi hilo na ni hatari sana,” alisema Askofu Shoo.
Aliongeza: “Kijana unaanza kunywa pombe kali yenye alcohol (kilevi) asilimia 48 na kuendelea, unaanza na miaka 25 nakuhakikishia hutafika miaka 50, ini litakuwa limekwisha, ninawaonya vijana acheni matumizi ya pombe kali.”
Vijana kufunga ndoa
Wakati huohuo, Askofu Askofu Ludovick Minde wa jimbo katoliki la Moshi, amezitaka jumuiya ndogo ndogo za kanisa hilo kuangalia namna ya kuwasaidia vijana wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa kuhakikisha wanafunga ndoa.
Askofu Minde aliyasema hayo jana wakati akihubiri katika Parokia ya Kristu Mfalme, Moshi mjini huku akihimiza kuchanga fedha ili kuwasaidia kutoka hali ya dhambi.
“Kuna vijana ukiwauliza masuala ya sakramenti ya ndoa wanakwambia bado kidogo tu baba askofu, bado kidogo mpaka lini? Unangoja nini? Jumuiya ndogondogo naomba muangalie hawa vijana kama ni mambo ya fedha tuwachangie, Yesu ni mkubwa kuliko fedha, tuwachangie watoke kwenye giza,” alisema Askofu Minde.
Aliongeza: “Hapo kwenye ndoa utata unatoka wapi kama mnapendana si mfunge ndoa, sasa unakaa miaka sita wengine miaka 12 unangoja nini yaani, ukiulizwa bado kidogo baba Askofu unangoja nini? Amua sasa, kwa hiyo lazima tuondokane na giza, yanatuchosha kwenye utakatifu.”
Imendikwa na Jesse Mikofu (Zanzibar), Peter Elias na Nasra Abdallah (Dar), Saada Amir (Mwanza), Suzy Butondo (Shinyanga), Robert Kakwesi (Tabora), Ernest Magashi (Geita), Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi), Habel Chidawali na Ramadhan Hassan (Dodoma), Burhani Yakub na Rajabu Athumani (Tanga), Janeth Mushi (Arusha) na Sanjito Msafiri (Kibaha).