Askofu Gwajima, Silaa watiwa hatiani na Bunge

Muktasari:

  • Wabunge hao inaelezwa mbele ya kamati kuwa walikuwa na jeuri na kiburi mbele yao lakini hawakutaka kujutia makosa yao.

Dodoma. Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge limetoa azimio la kuwasimamisha mikutano miwili wabunge Askofu Josephat Gwajima na Jery Silaa kwa kuwatia hatiani.


Wabunge hao wiki iliyopita waliitwa mbele ya kamati hiyo kwa kuhojiwa kuhusu matamshi waliyotoa nje ya Bunge.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka ameliambia Bunge kuwa wawili hao ni wakaidi na wajeuri lakini ni watu ambao hawakutaka kujutia kauli zao.


Mwakasaka amesema wabunge hao mbali na adhabu walizopewa, lakini wanatakiwa kuangaliwa kuhusu mienendo yao nje ya Bunge.

Hukumu ya Askofu Gwajima na Silaa mikononi mwa Bunge


Kwa upande wa Askofu Gwajima amepewa adhabu hiyo huku alitakiwa kuchunguzwa na vyombo vingine kutokana na kinachodaiwa ni uchochezi na upotoshaji.


Kamati imependekeza Gwajima pia kufikishwa mbele ya kamati ya chama chake CCM ili akahojiwe huko kuhusu mwenendo wake.

Soma: Askofu Gwajima, Silaa waondolewa ujumbe Kamati ya Bunge
Kwa upande wake Silaa kamati imependekeza asimamishwe mikutano miwili lakini avuliwe uwakilishi wa Bunge la Afrika (PAP) kwa madai anaweza kusema uongo huko.


Kilichomponza Silaa ni kauli yake kuwa wabunge hawalipi kodi katika mishahara yao jambo lililoelezwa ni uongo kwani wabunge wanalipa kodi.


Kwa upande wa Askofu Gwajima ameponzwa na kauli zake alizotoa kanisani Julai 25,2021, Agosti Mosi, Agosti 8 na 15,2021 kuhusu suala la chanjo.