Hukumu ya Askofu Gwajima na Silaa mikononi mwa Bunge

Muktasari:

  • Wabunge hao walihojiwa na kamati hiyo kwa agizo la Spika wa bunge Job Ndugai Kwa tuhuma za kusema uongo na kushusha hadhi ya Bunge.

Dodoma. Sakata la wabunge Askofu Josephat Gwajima na Jerry Silaa limetua bungeni na leo Jumanne mchana mbivu na mbichi itajulikana kuhusu hukumu yao.


Mbunge wa Viti Maalum, Shally Raymond amewasilisha taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu wabunge hao.


Hii ni mara ya kwanza katika Bunge la 12 kamati kutoa taarifa yake mbele ya Bunge kwa wabunge waliohojiwa ingawa mbunge wa kwanza kuitwa mbele ya kamati hiyo alikuwa mbunge wa viti maalum, Felista Njau lakini taarifa yake haijawahi kusomwa hadharani.

Kanuni za Bunge zinatoa nafasi kwa Bunge kupokea taarifa kwanza kabla ya kuisoma na kuijadili kwa wabunge wote, hivyo baada kamati hiyo itawasilisha taarifa kamili na kujadiliwa bungeni.

Hukumu ya Askofu Gwajima na Silaa mikononi mwa Bunge


Shally ameanza kuwasilisha taarifa ya Mbunge wa Kawe, Askofu Gwajima ambaye alisema anatuhumiwa kwa makosa ya kusema uongo na kushusha hadhi ya Bunge.


Kwa upande wa Silaa amesema miongoni mwa tuhuma zake ni kuchonganisha wananchi na Bunge.

Wawili hao waliitwa mbele ya kamati mwanzoni mwa wiki iliyopita  ambao kila mmoja alihojiwa kwa siku mbili tofauti huku kukiwa na vioja vya kukataa viti walivyopangiwa na wakati mwingine kuhojiwa wakiwa wamesimama.


Hukumu ya kamati hiyo huwa ni mapendekezo ya mbunge kusimamishwa vikao kadhaa na kutolipwa posho.
Katika Bunge la 11, miongoni mwa waliopitiwa na adhabu hiyo walikuwa Godbles Lema, Halima Mdee, Zitto Kabwe na Ester Bulaya.