Askofu Shoo ataka kanisa liongozwe kwa kanuni kuepuka migogoro

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo
Muktasari:
- Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, amesema baadhi ya Dayosisi za kanisa hilo zilipuuza misingi ya utawala bora na demokrasia na kujikuta wameingia katika migogoro ambayo mingine ziligusa kanisa zima.
Arusha. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo,amelitaka kanisa hilo liongozwe kwa misingi ya kanuni,sheria na taratibu ambazo wamejiwekea ili kutokuingia katika matatizo na migogoro.
Askofu Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo, amesema kumekuwepo na baadhi ya Dayosisi chache za kanisa hilo ambazo misingi ya utawala bora na demokrasia ilipuuzwa na kujikuta zikiingia katika migogoro.
Mkuu huyo wa kanisa ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 23,2023,akitoa taarifa ya muktasari ya utekelezaji katika mkutano mkuu wa 21 wa kanisa hilo unaofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira,kinachomilikiwa na kanisa hilo.
Amesema kuwa migogoro hiyo iliyotokea katika baadhi ya dayosisi ilikuwa, kupanuka na kugusa kanisa zima, akitolea mfano Dayosisi ya Kusini na Jimbo lake la Mufindi, Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (Lushoto) na Dayosisi ya Konde.
"Niwaombe kanisa letu liongozwe kwa misingi ya kanuni,sheria na taratibu ambazo tumejiwekea na tukitunza hizo mimi sioni sababu ya kauingia katika matatizo,niimeshuhudia katika dayosisi nyingi zikiendesha shughuli zake na kubadili aina ya viongozi kwa njia ya demokrasia kufuata amani na utulivu," amesema.
"Zimekuwepo dayosisi chache ambazo misingi ya utawala bora na demokrasia ilipuuzwa kwa hiyo kujikuta zikiingia katika migogoro na baadaye migogoro hiyo kupanuka na kugusa kanisa zima. Tunamshukuru Mungu kwamba Kanisa kupitia Halmashauri Kuu, tulishirikiana na dayosisi husika na kutatua migogoro hiyo," amesema.
Askofu Shoo amesema kuwa mambo madogomadogo ambayo yamebaki yanaendelea kushughulikiwa na dayosisi hizo na kuwa zipo dayosisi zingine zilizopata migogoro ya ndani lakini ilitatuliwa kabla ya kusambaa sana kama ilivyokuwa kwa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Dayosisi ya Konde.
"Tunamshukuru Mungu ametuwezesha na mimi niseme hata yale mliyosikia ya kule Mtwara, Mungu kwa rehema yake amerudisha roho ya utulivu na tunaomba tutunze hilo. Wajumbe niseme tu neno hili tukizidi kumtegemea Mungu, tukizidi kulitii neno lake, tutizidi kushikamana kwa umoja kwa upendo na uaminifu kama Kanisa moja la KKKT, sina mashaka kwamba yeye Mungu wetu atatufanikisha katika yote hata yale yanayoonekana kuwa magumu," amesema Askofu huyo.
"Nishukuru dayosisi zote, Serikali na taasisi zake jinsi mlivyoniombea katika miaka nane niliyohudumu mmeniombea na kunitia moyo kwa njia mbalimbali nitoe shukrani nyingi kwa hayo yote miliyonifanyia na kwa kweli mmenifanya kuwa mnyenyekevu zaidi,"
Kuhusu miaka 60 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo amesema mafanikio makubwa wanayojivunia ni pamoja na kushiriki kazi na huduma mbalimbali japo pia kanisa lilipita katika migogoro na changamoto nyingi za wapinzani wa kazi ya Mungu wengine wakitoka ndani ya kanisa hilo.
"Mambo mengi yametokea na mengine kuchochewa zaidi na watu wenye kudharau na kukatisha tamaa kuendeleza kazi za Mungu na juhudi za kuimarisha umoja kwenye kanisa letu, tumeshuhudia migogoro kadhaa hata baadhi yetu wakijitokeza kudhihaki na kupinga waziwazi maamuzi na maelekezo halali ya kanisa letu lakini katika yote hayo tumeona Mungu kwa neema yake na ametuvusha," amesema mkuu huyo.
Amesema kanisa hilo limeendelea kukua na kwamba katika mkutano mkuu wa 20 walikuwa na washarika milioni saba ila kwa mwaka huu wamefika milioni 8.5 na kuwa limeendelea kutoa huduma mbalimbali ikiwemo za kijamii katika sekta za afya na elimu.
Kabla ya kufanyika mkutano mkuu huo leo, jana halmashauri kuu ya kanisa hilo imekaa ambapo kesho mkutano mkuu huo unatarajia kufanya uchaguzi wa mkuu wa kanisa.