Auawa na waombolezaji akizika mtoto wake

Muktasari:
Mkazi wa Nyambale kijiji cha Busanda Wilaya ya Geita, Doto Lubapula (58) ameuawa na waombolezaji wakati wa maziko ya mtoto wake aliyeugua ugonjwa wa kuvimba tumbo wakimtuhumu kumuua kwa ushirikina.
Geita. Mkazi wa kitongoji cha Nyambale kijiji cha Busanda Wilaya ya Geita, Doto Lubapula (58) ameuawa na waombolezaji kwa kumpiga na silaha za jadi wakimtuhumu kumuua mtoto wake aliyefariki baada ya kuugua ugonjwa wa kuvimba tumbo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea Novemba 24, 2023 wakati waombolezaji hao wakiwa kwenye mazishi ya mtoto wake Vicent Mnakwavi (35) aliyekua anaumwa ugonjwa wa kuvimba tumbo.
“Siku hiyo saa 8 mchana wakiwa mazikoni wakaanza minong’ono wakimtuhumu kuwatoa kafara watoto wake kwa imani za kishirikina, wakaanza kumzonga watu wema walijitahidi kuzuia lakini wakazidiwa… watu wakaanza kumpiga na mawe na vitu vyenye ncha kali, wakamjeruhi mwili wake na kufariki”amesema Maro
“Kiini cha tukio hilo ni imani za kishirikina wakimtuhumu kuwaua watoto wake kwa kuwa huyu sio wa kwanza wengine wawili walishafariki kwa ugonjwa huo wa kuvimba tumbo na huyu aliyefariki juzi ni watatu”ameongeza
Amesema kufuatia tukio hilo watu nane wanashikiliwa na Polisi kwa uchunguzi na watafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu shtaka linalowakabili ambapo pia amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Maro amewataka wananchi kuacha kuamini ushirikina na inapotokea kifo ni vema wakafuata taratibu ikiwemo kuomba uchunguzi wa kidaktari ili kupata ripoti itakayoeleza tatizo lililopelekea kifo cha marehemu.