Aweso ahamishia ofisi Duwasa, kisa mgawo wa maji Dodoma

Thursday January 21 2021
dawasopic
By Nazael Mkiramweni

Chamwino. Waziri wa Maji Juma Aweso amesema amehamishia ofisi yake katika ofisi ya Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira mjini Dodoma (Duwasa) kwa lengo la kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Waziri Aweso ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 21,2021 alipotembelea  miradi ya Duwasa ikiwamo visima vya maji na tanki la maji ambalo linatarajiwa kukamilika Februari 28,2021.

Amesema ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji ya muda mfupi  ameona kuna haja ya yeye kuhamishia ofisi yake katika ofisi ya mamlaka hiyo.

"Nikiwa karibu na Duwasa tutakuwa tunafanya kazi usiku na mchana ili kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi kwa ajili ya kuongeza kiwango cha maji. Kiwango tunachozalisha ni mita za ujazo 66,000  wakati mahitaji ni mita za ujazo 103,000, lazima tuongeze kasi," amesema Aweso.

Amesema tangi hilo linalotarajiwa kukamilika mwezi ujao litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 2.5 zitakazosaidia kukabiliana na changamoto ya maji.

Kwa upande wake meneja ufundi na usanifu Duwasa, Kashilimu Mayunga amesema gharama ya mradi huo ni Sh998 milioni.

Advertisement

Amesema mradi huo ambao unatekelezwa na Suma JKT unatarajiwa kukamilika kwa muda uliopangwa na utakuwa ni suluhisho la changamoto ya maji wilayani Chamwino.


Advertisement