Balozi Kairuki: China haina mpango kufungua vituo vya polisi Tanzania

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki
Muktasari:
- Siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kuripoti kuwa China ina mpango wa kufungua vituo vya polisi nchini, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amekanusha taarifa hizo akisema hazina ukeli.
Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema kuwa hakuna mpango wa China kufungua vituo vya polisi nchini.
Balozi Kairuki amesema hayo jana Jumatano Oktoba 20, 2022 ikiwa zimepita siku chache tangu baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kuripoti kuwa China ina mpango wa kuanzisha vituo vya polisi katika mataifa matatu Afrika ikiwamoTanzania.
Amesema “Sisi kama Tanzania hatuna mkataba wowote wa mahusiano ya kipolisi ambayo yanatuletea kufungua vituo vya polisi kama ilivyodaiwa wala hakuna mpango wowote. Hatujaomba, wala wao hawajatuomba kufanya hivyo,” amesema
“Niwahakikishie taarifa hizi sio za ukweli na Watanzania wazipuuzie” amesisitiza Balozi Kairuki akikanusha ripoti hizo.
China ina ushirikiano wa kipolisi na baadhi ya nchi duniani, ambapo mapema kwaka 2022 China ilifungua kituo cha polisi katika mji mmoja nchini Italia, kwa lengo la kuwasaidia watalii wengi wanaotoka China.
Hata hivyo, Balozi huyo amesema kuwa sio jambo jipya kwa taifa moja kufungua vituo vya polisi katika nchi nyingine akisema kuwa utaratibu huo upo duniani.
Amesema kuwa utaratibu huo unahitaji makubaliano maalumu baina ya nchi mbili kwa madhumuni mahususi.