Bandari ya Mtwara ya pili kwa kutoa huduma nchini

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Bandari ya Mtwara inashika nafasi ya pili kwa kutoa huduma ya makasha, ikitanguliwa na bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza leo Septemba, 15,2023 mkoani Mtwara, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Waziri huyo amesema katika historia ya bandari hiyo haikuwai kuhudumia makasha, lakini katika mwaka wa fedha ulioisha, makasha 51860 yalianza kuhudumiwa ikiwa ni historia tangu kuanzishwa kwake.
“Serikali iliwekeza katika kuboresha bandari ya Mtwara kwa kujenga gati yenye urefu wa mita 300 na kina cha maji mita 13 na tulitumia Sh167 bilioni na Serikali ilituongezea Sh51 bilioni za kuendelea kuiboresha maeneo mengine,” amesema.
“Baada ya ukarabati na uwekezaji huo na kuongeza vifaa vya kisasa bandari ya Mtwara imefanya mageuzi makubwa, kwani kabla ya uwekezaji huo, bandari ilikuwa na uwezo wa kuhudumia mizigo tani 592,363 kwa mwaka, na kwamba sasa inahudumia tani milioni 1.628 kwa mwaka na haijawai kutokea,” amesema.