Masuala nyeti ziara ya Rais Mtwara

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abass
Muktasari:
- Yafuatayo ni miongoni mwa masuala muhimu kwa wananchi wa Mtwara, wakati Rais Samia Suluhu Hassan, akianza ziara yake ya kwanza tangu awe kiongozi wa nchi Machi, 2021, mamlaka aliyoyapata kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Mtwara. Rais Samia Suluhu Hassan leo Septemba 14 anatarajiwa kuwasili mkoani hapa alasiri tayari kuanza ziara yake ya siku nne ambayo itafikia kikomo Septemba 17, 2023; huku mkoa ukijivunia bei nzuri ya mazao, ambayo inatokana mazingira bora ya ufanyaji biashara.
Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji), Nanjiva Nzunda, amesema kuwa kwa sasa Mtwara inajivunia mavuno na bei nzuri ya msimu uliomalizika wa ufuta na minada inayoendelea ya zao la mbaazi.
Katika msimu ulioisha wa ufuta, mkoa umekusanya na kuuza ufuta tani 17, 844; huku lilikuwa tani 15,000 na kwamba mauzo hayo, yameingiza Sh66.3 billioni, ikilinganishwa na msimu uliopita ambapo tani 9,523 zenye thamani ya Sh29.6 bilioni ziliuzwa.
Wakati bei ya chini msimu uliopita ilikuwa Sh3, 083 kwa kilo, huku ile ya juu ikifikia Sh3, 202; katika msimu wa mwaka huu bei ya chini Sh3, 665 na juu ni Sh3, 967.
“Tunaishukuru Serikali, bei ni nzuri, tumeridhika na tunashukuru kuliingiza zao hili la ufuta katika mfumo wa stakabadhi ghalani,” amesema mkulima wa Wilaya ya Masasi, John Mrope.
Kwa mara ya kwanza msimu huu, zao la mbaazi limeanza kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo hadi sasa minada minne imeshafanyika na tani zaidi ya 12,000 zimeuzwa katika malengo ya kukusanya na kuuza tani 15,000.
Bei ya juu kwa kilo moja ya mbaazi ni Sh2, 139 huku ya chini ikiwa imebaki kuwa Sh2, 000. Kabla ya mafanikio haya yaliyotokana na kufunguliwa kwa minada kwa zao hilo, awali mbaazi iliuzwa hadi Sh300 kwa kilo moja.
“Kabla ya minada kuanza mwaka huu wakulima waliuza kilo moja ya mbaazi hadi Sh1, 300,” amesema Mshauri wa Kilimo Mkoa, Ally Linjenje.
Kwa muda mrefu Mkoa wa Mtwara ambao unazalisha zaidi ya asilimia 60 ya korosho yote nchini, ulikuwa ni tegemezi kwa zao hilo pekee.
Hata hivyo, uzalishaji na bei ya kororsho, imekuwa ikiporomoka, jambo ambalo lilisababisha uchumi wa mkoa kuyumba, na maisha kuwa magumu.
Mathalan, katika msimu wa 2021/2022; mkoa ulijiwekea lengo la kuzalisha tani 162,400 za korosho, lakini hadi msimu unaisha, zilikusanywa na kuuzwa tani 130, 297. Wakati msimu wa nyuma yake, (2020/2021), zilizalishwa tani 118,250 zenye thamani ya Sh282.35 bilioni.
Rais anafika Mtwara kwa mara kwanza, wakati ambapo taarifa kutoka Bodi ya Korosho nchini (CBT), zinaonyesha kuwa bei ya korosho daraja la kwanza imeshuka kutoka Sh4, 128 msimu wa 2017/2018 hadi Sh2, 200 msimu wa 2022/2023.
Na hapa ndipo, Linjenje ambaye ni msahuri wa kilimo mkoa huo anasema: “...jitihada za mkoa zilianza tokea mwaka 2019, kuhamasisha wananchi kulima mazao tofauti na korosho ikiwemo ufuta na sasa wanatarajia kuingiza zao la karanga katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
Bandari ni eneo lengine la kiuchumi ambalo wakazi wa Mtwara wamekuwa wakilitolea macho, na hasa baada ya kushindwa kusafirisha korosho katika misimu miwili iliyopita, huku wananchi walio wengi wakiamini kwamba kuna hujuma.
Hata hivyo ugeni wa Rais Samia unaingia Mtwara, huku Tayari bandari hiyo ikiwa imeishaanza kusafirisha makasha ya korosho toka mwzi Aprili mwaka huu.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kijavara, hadi sasa kuna makasha zaidi ya 10, 000 katika bandari hiyo.
“Tuko tayari kuanza kusafirisha korosho zote za msimu huu na bidhaa nyingine zozote, miaka ya nyuma tulishindwa kwa sababu hatukuwa na meli wala makasha,” amesema Juma.
Licha ya mafanikio hayo, kwa upande wa Mwandishi Mturi, yeye anasema anatamani kusikia kauli ya Rais, kuhusu ni kwa namna gani anaziunganisha nchi tatu za Tanzania, Msumbiji na Malawi ili ziweze kutumia bandari hiyo, na hivyo kuleta unafuu wa maisha kwa wakazi wa Mtwara.
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara, Bryson Mshana, anadhani bado korosho ina sehemu kubwa katika uchumi wa mkoa huo, hivyo anatamani kusikia maelekezo ya Rais kwa CBT, na Wizara ya Kilimo ambayo kimsingi ndiyo yenye mamlaka na wajibu wa kusimamia korosho.
Mshana anatamani kusikia maelekezo hayo yakijikita kwenye mikakati endelevu ya kulikuza zao hili kwa maana ya kilimo chake, lakini pia namna bora ya kupata masoko bora.
“Kwa sasa kinachofanyika nguvu kubwa imeelekezwa katika pembejeo na elimu ya kilimo lakini ya elimu ya masoko haitolewi, wakulima wanatakiwa kujua soko limekaaje huko duniani,” amesema Mshana.
Tukirejea kwa habari ya hali ya hewa kisiasa, Rais anaingia Mtwara akiwa na amezingirwa na nguvu ya wananchi, baada ya wao kutokubaliana na kile kilichofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Tatu Saidi, na hivyo kupelekea Rais kuwatimua kazi.
Hatua hii ya kuwatimua kazi viongozi hao, ilipokelewa kwa shangwe, hivyo Rais anaingia Mtwara huku wananchi wakimsubiri shujaa wao kwa hamu, ili kama wana kero zingine basi waweze kuziwasilisha wakiamini kuwa zitafanyiwa kazi.
“Kisiasa Rais amejiwekea kwamba yeye ni wa wananchi wote, atahamasisha watu waendelee kufanya kazi bila upendeleo na wananchi wameelewa kwamba maendeleo ni haki yao bila kujali itikadi za kisiasa,” amesema Mshana.