Barabara ya mwendokasi Gerezani-Mbagala kukamilika Aprili

Muktasari:

  • Serikali yasema barabara ya mabasi yaendayo haraka ya kilomita 20.3 kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi tatu itakamilika Aprili mwaka huu.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema awamu ya pili ya ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi tatu, utakamilika Aprili.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 20.3. Pia ujenzi wa vituo 27 vya mabasi ya mwendo wa haraka, barabara za juu tatu na njia za maji za chini zenye urefu wa kilomita 40.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Febuari 27, 2023 wakati akikagua ujenzi wa awamu ya tatu ya barabara ya kiwango cha zege ya mabasi yaendayo haraka kutoka Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto yenye urefu wa kilomita 23.3 utakaogharimu Sh231 bilioni.

“Hivi karibuni tunakwenda kumaliza ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka awamu ya pili. Katikati ya Aprili itakamilika kwa asilimia 100 tulipata changamoto ya daraja la juu kwa sababu tulichelewa kuwapa eneo.

“Hii ya awamu ya tatu itakamilika Machi mwakani, niwaambie tu wakazi wa Dar es Salaam, kabla ya uchaguzi mambo yatakuwa mazuri,” amesema Profesa Mbarawa.

Kuhusu ujenzi wa awamu ya tatu, Profesa Mbarawa amesema mkandarasi amejipanga vizuri kutekeleza jukumu hilo na ametembelea ghala lililopo Buza kuoana maandalizi yake.