Baraza latambua ‘massage’ kama tiba asili

Muktasari:
Kupitia Sheria ya Tiba za Asili, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala limepewa mamlaka ya kusimamia utoaji wa huduma za ukandaji na uchuaji misuli, kwa lengo la kuhakikisha kuwa wataalamu wa huduma hizo wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mipaka, maadili na miongozo rasmi ya kitaalamu.
Morogoro. Kwa mujibu wa Sheria namba 23 ya mwaka 2002 ya Tiba za Asili na Tiba Mbadala, huduma za ukandaji na uchuaji misuli zinatambuliwa kama sehemu ya tiba za asili, na maeneo yanayotoa huduma hizo yanahesabiwa kuwa vituo vya tiba asili.
Vilevile, wataalamu wa huduma hizo wanatambulika kama sehemu ya waganga wa tiba asili.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Profesa Joseph Otieno, wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu Sheria ya Tiba Asili na jinsi baraza hilo linavyotekeleza majukumu yake.
Profesa Otieno amesema kuwa kupitia sheria hiyo, Baraza lina mamlaka kamili ya kusimamia utoaji wa huduma za tiba asili pamoja na vituo vinavyotoa huduma hizo.
Amesisitiza kuwa hata wataalamu wa kukanda na kuchua misuli wanapaswa kutambua kuwa huduma wanazotoa ziko chini ya usimamizi wa baraza.
"Wale wataalamu wanaowakanda na kuwachua watu misuli kwenye kazi hiyo wanahusisha dawa ama mafuta yaliyotengenezwa na mitishamba ama mimea tiba, lakini pia wanagusa viungo mbalimbali vya mtu ambaye wanamwita ni mteja," amesema Profesa Otieno.
Hata hivyo Profesa Otieno amesema kuwa baraza linatambua huduma ya kukanda na kuchua misuli kama ni tiba mbadala, hivyo kwa kushirikiana na vyuo vya tiba hapa nchini wamepanga kutoa mafunzo kwa wataalamu wa kukanda na kuchua misuli ili wajue sheria na mipaka yao katika utendaji wa kazi zao.
"Lazima hawa wataalamu wa kukanda na kuchua misuli wapewe elimu kwa sababu wanashughulika na mwili wa mtu na wanagusa viungo mbalimbali vya mwili, hivyo ni vyema wakatambua mipaka yao wanapofanya shughuli hiyo," amesema Profesa Otieno.
Kutokana na sheria hiyo ya kuwatambua wataalamu wa kufanya wanaokwenda na kuchua misuli baraza limepanga kufanya ufuatiliaji kwenye maeneo yanayotoka huduma hiyo ili kuona huduma huyo haikiuki sheria za tiba asili.
Akifafanua kuhusu baadhi ya makatazo yaliyomo kwenye Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, Profesa Joseph Otieno amesema kuwa ni marufuku kwa mganga wa tiba asili kugusa au kushika maeneo nyeti ya mwili wa mgonjwa au mteja, iwe kwa hiari au kwa lazima.
Aidha, sheria hiyo pia inapiga marufuku matumizi ya vifaa vyenye ncha kali, ikiwemo sindano, katika kutoa matibabu.
Mmoja wa wataalamu wa kukanda na kuchua misuli katika Manispaa ya Morogoro, aliyejitambulisha kwa jina la Mina, amesema kuwa huduma hiyo anayotoa inafanyika kwa hiari ya wateja na hutolewa katika saluni rasmi anakoajiriwa.
"Mimi sitoi huduma hii majumbani, nafanyia hapa kwenye kituo changu cha kazi. Sijasomea chuo rasmi, ila nimejifunza kupitia wataalamu mbalimbali niliowahi kufanya nao kazi hapa Morogoro na Dar es Salaam.
“Kwa sasa nami ni mtaalamu, na wapo wateja wangu ambao wakinikosa hapa kituoni huondoka bila kuhudumiwa na mwingine," amesema Mina.
Kuhusu uhalali wa huduma hiyo, Mina alikiri kutokuwa na uelewa kama ni sehemu ya tiba asili au la.
"Sijui kama hii huduma ni ya asili au ya Kizungu, maana mafuta na dawa tunazotumia tunazinunua kwenye maduka ya kawaida, siyo ya mitishamba. Hata kuhusu hilo Baraza la Tiba Asili, silijui kabisa," ameeleza.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kutoa huduma hiyo, Mina amesema baadhi ya viungo vya mwili lazima viguswe wakati wa uchuaji kama vile mabega, shingo, mgongo, kiuno, mapaja na miguu.
"Kwa sababu huduma hii inahusisha uchuaji wa misuli na unyooshaji wa viungo, mteja hupewa ushauri wa kuvua baadhi ya nguo kwa hiari yake ili kupakwa mafuta. Si lazima avue zote mara moja, anaweza kuvua shati ili achuliwe mgongo na shingo, kisha baadaye suruali na kubaki na kaptura fupi ili achuliwe mapaja na miguu," amesema.
Mina amesisitiza kuwa wataalamu wengi wa uchuaji misuli wanafanya kazi hiyo kwa uadilifu na maadili ya hali ya juu.
"Wapo wanaotufikiria vibaya, hasa sisi wanawake. Wengine hudhani tunawatega wateja kimapenzi. Lakini binafsi huwa sikubali. Hii ni kazi kama nyingine. Nakula na kumsomesha mtoto wangu kwa kupitia kazi hii," ameeleza kwa msisitizo.
Hata hivyo, ameonesha utayari wa kupatiwa mafunzo rasmi kutoka Baraza la Tiba Asili ili kuongeza ujuzi na weledi katika kazi yake.
Awali, Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Lucy Mziray amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 60 ya wagonjwa katika maeneo mbalimbali, hasa vijijini, huanza kutafuta tiba kupitia tiba asili kabla ya kwenda hospitali.
Kwa upande wake, Ofisa wa Baraza hilo, Martin Mgongwa ameonya kuwa licha ya kuwepo kwa sheria za kusimamia tiba za asili, bado wapo baadhi ya waganga wanaokiuka kwa kuuza dawa kiholela katika mikusanyiko ya watu, ndani ya mabasi na kandokando ya barabara.