Benki ya maendeleo Afrika yaahidi kufadhili miradi Tanzania

Friday June 11 2021
benki pic
By Mariam Mbwana

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo  Afrika (AFDB) imesema itaendelea kufadhili miradi ya maendeleo nchini Tanzania ikiwemo miradi mipya.

 Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Jaffar Haniu leo Ijumaa Juni 11,  2021 imemnukuu rais wa benki hiyo, Dk Adesina Akinumwi wakati akiwasiliana kwa njia ya simu na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Dk Akinumwi ameahidi AFDB itatoa ufadhili kwa Tanzania ili ianzishe benki za wajasiriamali zitakazotoa mikopo kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi na wanaojihusisha na shughuli za kilimo.

Amesema mikopo hiyo itawezesha kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuwaongezea kipato.

“AFDB itatoa ufadhili kwa Tanzania ili iweze kuanzisha benki za wajasiriamali zitakazotoa mikopo kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi na wanaojihusisha na shughuli za kilimo. Mikopo hii itawezesha kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuwaongezea kipato,” amesema Dk Akinumwi.

Dk Akinumwi amemualika Samia kwenye mkutano wa wawekezaji utakaowakutanisha wawekezaji wakubwa pamoja na kubainisha kuwa benki hiyo imetenga Dola 5 bilioni za Marekani kwa ajili ya kusaidia wanawake na ameiomba Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa uwezeshwaji wa wanawake kiuchumi jambo alilodai kuwa Rais Samia ameliafiki.

Advertisement

Pia, ameahidi kuleta wataalam wa benki hiyo wakutane na wataalam mbalimbali nchini kupitia miradi inayofadhiliwa na benki hiyo na kujadili fursa za kuanzisha miradi mipya.

Kwa upande wake Rais Samia  amemshukuru Dk Akinumwi ameshukuru benki hiyo kwa kufadhili  miradi mingi ya maendeleo nchini ikiwemo ile inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa.

Pia, amefurahishwa na mradi wa benki hiyo utakaofadhili vijana wanaojihusisha na kilimo pamoja na wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi kwani utawawezesha vijana wengi wa Tanzania kuzalisha mali.

Advertisement