Bosi wa Tigo Tanzania aaga

Bosi wa Tigo Tanzania baaga

Muktasari:

  • Ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Hishem Hendi kutangaza kuachana na kampuni hiyo baada ya kupata nafasi nyingine Hispania, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari ametangaza kuondoka nchini.

Dar es Salaam. Ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Hishem Hendi kutangaza kuachana na kampuni hiyo baada ya kupata nafasi nyingine Hispania, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari ametangaza kuondoka nchini.

Taarifa za kuondoka kwa Karikari zilizoenea tangu Ijumaa iliyopita zilithibitishwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tigo, Balozi Ami Mpungwe alipozungumza na gazeti hili.

“Mkataba wake unaisha mwezi huu, alinijulisha mapema kwamba hataendelea na mkataba wake. Ataondoka mwishoni mwa Septemba hii,” alisema Balozi Mpungwe.

Tofauti na Hendi aliyeaga Agosti 4, mwajiri wake akisema anakoelekea, Balozi Mpungwe hakuwa na uhakika wa anakoelekea Karikari na alipoulizwa Karikari mwenyewe hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza kwa kuwa alipopigiwa simu alikata na kutuma ujumbe mfupi: “Will call back (nitakupigia)” lakini mpaka tunaenda mitamboni hakufanya hivyo.

Karikari anaondoka Tigo baada ya kufanya kazi na kampuni hiyo kwa takriban miaka saba, ikiwamo mitano aliyodumu nchini.

Mkurugenzi huyo alianza kufanya kazi nchini akiwa ofisa mkuu wa fedha Tigo, kuanzia Aprili 2016 hadi Mei 2017.

Kuanzia Juni mwaka huo aliteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ya pili kwa kuhudumia wateja wengi wa mawasiliano nchini.