Bosi wa zamani KCBL kizimbani

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro imemfikisha mahakamani aliyekuwa mhasibu wa  Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL),Ombeni Masaidi  akikabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi namba 10 la mwaka 2019.

Moshi. Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro imemfikisha mahakamani aliyekuwa mhasibu wa  Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL),Ombeni Masaidi  akikabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi namba 10 la mwaka 2019.

 Mhasibu huyo amefikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  Moshi leo Ijumaa Juni 11, 2021 na kuunganishwa na wenzake wawili waliokuwa wafanyakazi wa benki hiyo, Joseph Kingazi na Elizabeth Makwabe.

Akitoa taarifa kwenye vyombo vya habari mkuu wa Takukuru mkoani Kilimanjaro, Frida Wikesi amesema Ombeni amekamatwa mkoani Dodoma baada ya kutoroka miaka miwili iliyopita.

Amebainisha kuwa anakabiliwa na makosa mengine ikiwemo kuisababishia Serikali hasara pamoja na kughushi nyaraka mbalimbali za Serikali.

"Ombeni atakuwa ni mshtakiwa wa tatu na alipojua anatafutwa na Takukuru alitoroka kujaribu kukwepa mkono wa sheria, maofisa wetu wamemkamata jijini Dodoma,” amesema Wikesi.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi inaendeshwa na wakili wa Takukuru, Rehema Mteta kwa kushirikiana na mawakili wengine wa Serikali.

Oktoba 2019  Kingazi alifunguliwa mashtaka 32 ya uhujumu uchumi ikiwamo kudaiwa kuiba Sh3 bilioni huku Januari 2020,  Makwabe alifunguliwa mashtaka ya zaidi ya Sh3 bilioni.