Bulaya ataka Serikali itibu waraibu wa dawa za kulevya

Muktasari:

  • Mbunge Ester Bulaya mbali na kutaka Serikali itibu waraibu wa dawa za kulevya, pia amesema takwimu zinazotumiwa na Serikali kuhusu watumiaji wa dawa za kulevya zimepitwa na wakati.

Dodoma. Suala la uraibu wa dawa za kulevya limemuibua Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya aliyetaka Serikali ya Tanzania kuwatibu waraibu wa ulevi huo kwa kuwa ni mzigo kwa familia na Serikali kutokana na magonjwa wanayopata, kama ini na figo.

 Bulaya amesema hayo leo Alhamisi, Aprili 4, 2024 wakati akichangia mjadala bungeni kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025.

“Kuhusu dawa za kulevya, mimi nasema kila mara nina mdogo wangu ameathirika na yuko ‘sober’ ya Bagamoyo (mkoani Pwani). 

“Serikali lazima muwekeze kwenye kutibu, lengo la kuanzisha tume (zamani ilifahamika kama Tume ya Kuratibu Uthibiti wa Dawa za Kulevya Tanzania na sasa inaitwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya- DCEA), ilikuwa ni kuzuia, kukamata na kutibu waraibu wa dawa za kulevya.

“Mmejikita kwenye kukamata na sasa hivi mnakamata sana, mnajua kwa sababu gani, kwa taarifa ya Umoja wa Mataifa, huko duniani wazalishaji wa dawa za kulevya wameongezeka kwa asilimia 25, na hizo mnazozikamata ni ndogo, bado watu wanaingiza kimya kimya, vijana wetu wanaathirika,” amesema na kuongeza;

“Sasa wakati mnaendelea kupambana hakikisheni wale walioathirika mnawatibu na mkishawatibu mtapunguza magonjwa yanatokana na kutumia dawa za kulevya, watu wanaharibika ini, wanaharibika figo mwisho wa siku mnakuwa na mzigo mzito wa kuhudumia magonjwa ambayo yanatokana na dawa za kulevya,” amesema Bulaya.

“Haya ukienda kwa mfano MAT (Medication-Assisted Treatment) kliniki ya Mwanyamala (Dar es Salaam),   watu wanaokunywa dawa pale ni msongamano watu 1,500. Nenda Muhimbili 1,200 (Dar es Salaam), nenda kliniki ya Tanga zaidi ya watu 1,000, lakini walioathirika ambao kwa takwimu zilizopitwa na wakati ni 530,000. Watu 30,000 ni ambao wanajidunga, laki tano ni wale wanaovuta, wanalamba.  Sasa mnawezaje kupambana na takwimu za sasa?” amehoji Bulaya.

Akionyesha kama vile Serikali haifanyi chochote, amesema Serikali yenyewe mna ‘rehab’ moja (Kituo cha kusaidia warahibu wa dawa za kulevya). “Serious’, kwa tatizo kubwa namna hii, kweli halafu huku mnatupa taarifa mmekamata bangi, sijui nini bado kuna tatizo la msingi. Ndugu zangu ukiwa na mtu ambaye unamhudumia, mosi ‘future’ yake imeharibika, vingine ni mzigo wako.

“Leo kuna ‘sober house ziko 40’ (Nyumba za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya na ulevi wa. pombe), hizo ni za watu binafsi, lakini mnazisaidiaje, nyie Serikali hamna, tatizo ni kubwa, tatizo ni kubwa sana,” amesema Bulaya.

Kauli hiyo ya Bulaya ilimuibua Mnadhimu Mkuu wa Serikali bungeni, Jenista Mhagama ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kumpa taarifa Bulaya.

Mhagama amempa taarifa Bulaya kwamba kwa mujibu wa mikataba ambayo nchi imeridhia na kukubaliana kimataifa katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya, ni kushirikisha wadau mbalimbali na si kazi inayoweza kufanywa na Serikali pekee.

“Kwa hiyo tunachokifanya ‘sober house’ zinazoanzishwa na wadau, kila mwaka Serikali ndani ya Bunge imekuwa ikitenga bajeti ya kuzisaidia hizo ziweze kufanya kazi nzuri ya kuendelea kuwahudumia waraibu hao.

“Kwa hiyo ni lazima waheshimiwa wabunge tujue kwamba kazi inayofanywa na Serikali ni nzuri kwa kushirikiana na wadau hao ambao wamekuwa wakianzisha hizo ‘sober house’. Serikali inawajibika ipasavyo na ndio maana mmeona mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanafanikiwa na mheshimiwa Ester utakubaliana na sisi kazi nzuri inafanywa,” amesema.

Hata hivyo, Bulaya alikataa kuipokea taarifa hiyo akisema; “Siipokei kwa sababu kutenda ni jambo lingine, kupeleka ni jambo lingine.

“Mimi sisimami hapa bila kufanya utafiti, ugezitaja hapo data (takwimu), mimi ndio maana nimekutajia hapa. Zamani mlikuwa mnaweza kuwasaidia kuwalipia hata kodi miezi sita, sasa hivi hakuna, ni jambo la kupokea tu dada yangu, kwa sababu hili ni janga letu sote, kizazi kinaharibika, wastaafu wanung’unike, vijana nao,” amesema Bulaya.

Alichosema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye taarifa yake jana Jumatano alisema kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Serikali imepata mafanikio makubwa katika udhibiti na hadi kufikia Desemba 2023, jumla ya kilogramu milioni 1.96 za dawa za kulevya zilikamatwa kutoka kwa watuhumiwa 10,522.

“Aidha, dawa tiba zenye asiliya kulevya kilogramu 1.95 na lita 61.67 zilikamatwa. Kiasi hicho kilichokamatwa ni zaidi ya jumla ya dawa za kulevya zilizokamatwa nchini katika kipindi cha miaka 11 kuanzia mwaka 2012 hadi 2022 ambazo ni kilogramu 660,465.4.

“Mafanikio haya yameipa heshima nchi yetu kimataifa kwa kupewa tuzo mbalimbali kutokana na udhibiti ulioonyesha ufanisi mkubwa ndani na nje ya mipaka ya nchi.

“Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanikiwa kuteketeza ekari 2,389 za mashamba ya bangi katika mikoa ya Arusha ekari 1,093, Morogoro ekari 489, Mara ekari 807 na ekari 535 za mashamba ya mirungi katika Mkoa wa Kilimanjaro,” alisema.

Majaliwa pia alisema Serikali imefanya ukaguzi kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa biashara ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

“Ukaguzi huo ulifanyika katika maeneo mbalimbali 734 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza, Songwe, Shinyanga, Dodoma na Kilimanjaro.

“Halikadhalika, kupitia mifumo ya kielektroniki, Serikali ilifanikiwa kuzuia kemikali bashirifu kilogramu 157,738.55 na lita 1,000 zilizokuwa ziingizwe kinyume cha sheria ambazo kama zingechepushwa zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya,” alisema.

Majaliwa alisema pia juhudi hizo zimekwenda sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Uelimishaji Kuhusu Rushwa na Dawa za Kulevya utakaotumika kwenye Klabu za Kupinga Rushwa na Dawa za Kulevya Shuleni na Vyuoni; kukamilisha Sera ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2023 na kuanzisha maabara ya uchunguzi na sayansi jinai.