Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bunge kufanya maamuzi bima ya afya kwa wote

Muktasari:

Siku 40 tangu muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote usomwe kwa mara ya kwanza katika Bunge la Tanzania, muswada huo unatarajiwa kusomwa tena kesho na kuanza kujadiliwa na wabunge ili kupitishwa kuwa sheria kabla ya utekelezaji wa rasimu hiyo kuanza Julai 2023.

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania kesho linatarajiwa kuanza kujadili muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa mwaka 2022 utakaosomwa kwa mara ya pili na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Muswada huo unatua kwa mara ya pili bungeni ikiwa ni siku 40 zimepita tangu uliposomwa kwa mara ya kwanza Septemba 23, 2022.

Tangu Oktoba 19 mwaka huu, Kamati ya Kudumu ya Bunge Huduma na Maendeleo ya Jamii ilianza kupokea maoni ya wadau kuhusu muswada huo na kufanya marekebisho kadhaa kabla ya kupelekwa Bungeni ambapo utajadiliwa na wawakilishi wa wananchi (wabunge) na unatarajiwa kupitishwa katika Bunge hili la Novemba.

Kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano wa tisa wa Bunge, wabunge watajadili muswada huo kwa muda wa siku mbili yaani Novemba 2 na 3, 2022.

Hata hivyo wadau mbalimbali wamekuwa wakikosoa baadhi ya vifungu vilivyopo katika muswada huo.

Chama cha ACT Wazalendo kiliitaka Serikali kutourejesha bungeni muswada huo kutokana na mapungufu yaliyopo huku, Chadema nayo ikisema muswada huo hauna uhalisia kwa maisha ya sasa.

Oktoba 25 mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Ustawi wa Jamii wa chama hicho, Ashura Masoud alisema mfumo unaopendekezwa na muswada huo utakandamiza wananchi.

"Mfumo huu unaminya haki za watu na kusababisha mateso na maafa kwa wananchi. Mbadala wake ni kuondolewa au kuboreshwa vifungu vyote vya muswada vinavyowakandamiza wananchi," alisema.

Alitoa mfano wa kifungu cha 32 kinachoeleza ufungamanishaji wa huduma, akisema kinanyima raia haki zao za msingi na kuchochea umasikini kwa wananchi.

Hata hivyo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa mapendekezo ya maboresho katika miswada ya Sheria mitatu iliyopelekwa bungeni, ukiwemo wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, wakikosoa baadhi ya vifungu.

Baadhi ya vifungu walivyokosoa katika muswada ya Bima ya Afya kwa Wote ni pamoja na kifungu cha tatu kinachotoa tafsiri ya mtu asiye na uwezo bila kudadavua bayana ni yupi mtu huyo asiye na uwezo.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema kuwa kifungu hicho hakijaweka wazi sifa za kumtambua mtu huyo asiye na uwezo jambo linaloweza kuleta changamoto hapo baadaye.

Pia amegusia kifungu cha D 20(1) ambacho kinaweka takwa la lazima kwa mwajiri kuwasilisha jina la muajiriwa wake katika bima ya afya ndani ya siku 30 tangu alivyosaini nae mkataba.

Hata hivyo Mwananchi lilimnukuu Waziri wa Afya akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuhakikisha wanapeleka mapendekezo yao kabla ya muswada huo haujarudi tena Bungeni kujadiliwa na kuwa sheria.

“Mawazo, ushauri na maoni nini kiwepo au kisiwepo yanapokelewa na kamati, kama wana hoja wazilete kwenye kamati, sisi tutayajibu baada ya kupata taarifa ya kamati muswada bado upo ngazi ya kamati na Bunge na ndiyo linapokea maoni,” alinukuliwa Waziri Ummy Oktoba 25 mwaka huu.


Yaliyomo kwenye muswada

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote unazitaka mamlaka nane zinazotoa usajili, vibali, hati au leseni kwa waombaji kuzingatia kigezo cha uwepo wa uthibitisho wa uanachama katika skimu ya bima ya afya.

Mapendekezo hayo yamewekwa kufanyika kwa kuzingatia sheria zilizotungwa na Bunge, mamlaka zinazohusika na usimamizi au utoaji.

Muswada huo unazitaja mamlaka hizo kuwa ni zinazotoa leseni ya udereva, bima za vyombo vya moto, utambulisho wa mlipa kodi, usajili wa laini za simu, leseni ya biashara, hati ya kusafiria au viza, uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha tano, kidato cha sita na vyuoni na utoaji wa kitambulisho cha Taifa.

Kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika kanuni, mwajiri katika sekta ya umma na sekta rasmi binafsi atapaswa kumsajili mwajiriwa katika skimu ya bima ya afya ndani ya siku 30 tangu kuanza kwa mkataba wa ajira.

Kwa madhumuni ya upatikanaji wa kitita cha mafao ya msingi, kila mwajiri chini ya sekta ya umma na sekta binafsi atawasilisha katika skimu asilimia sita ya mshahara wa mwajiriwa na yeye atachangia nusu ya kiwango.

Muswada unaeleza Waziri kwa kushauriana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, ataainisha viwango vya uchangiaji kwa ajili ya sekta isiyo rasmi.

Pia ulipendekeza waziri, kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika, na kwa kupitia kanuni, ataweka utaratibu na namna ya utambuzi wa watu wasio na uwezo.