Bunge latakiwa kuwajibika kwa wananchi matarajio ya bajeti

Muktasari:

  • Kutopelekwa kwa fedha zilizopitishwa katika bajeti za kisekta kila mwaka kumetajwa kusababishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kushindwa kuisimamia Serikali ipasavyo.

Dar es Salaam. Kutofikiwa kwa matarajio ya wananchi katika bajeti zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kumeelezwa kuwa ni kulegalega kwa mhimili huo katika kuisimamia Serikali.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 7, 2023 na  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha NCCR, Nicholaus Peter katika mjadala wa Twitter Space unaoendeshwa na kampuni ya Mwananchi Communicationi,uliobeba mada ya ‘Matarajio Bajeti za kisekta zilizopitishwa na Bunge zinakidhi mahitaji ya wananchi?’

Peter amesema umasikini umetawala maeneo mengi ya nchi, huku Wabunge wakilifanya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa chombo cha kutetea Serikali ya CCM badala ya wananchi.

“Wabunge wengi wanaosiamama wanasifia Serikali badala ya kueleza changamoto za wananchi, tuna wabunge wanaolifanya Bunge lisiwajibike kwa wananchi.

“Kwa bahati mbaya wananachi wetu pamoja na katiba kuwaruhusu kuwawajibisha wawakilishi wao, bado hawana uelewa juu ya hilo,” amesema.

Peter amesema linahitajika Bunge ambalo sio la kuisifiasifia Serikali bali kuiwajibisha.

Ili kuipima Serikali, amesema ni lazima ieleze katika kutekeleza mipango yake ya maendeleo ndani ya miaka miwili, ndani ya miaka mitano, imeweza kuwatoa vipi watanzania katika umasikini.

Kwa upande wake Msemaji wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa chama cha ACT Wazalendo, Dk Nasra Nassoro, amesema suala la bajeti za kisekta kutokidhi mahitaji ya wananchi sio la leo lipo miaka yote na limekuwa kama nyimbo kila siku.

Dk Nasra amesema hii ni kwa kuwa bajeti inayoidhinishwa na bunge hakuna hata moja ambayo inatekelezwa kwa asilimia 100.

“Haya yanatokea kwa sababu Serikali haina vipaumbele, kwa kifupi tumekuwa tunabadilisha vipaumbele vyetu, tunashindwa kutekeleza miradi au kupeleka fedha zinakohitajika kwa sababu ya kutokuwa na mwelekeo,” amesema Msemaji huyo.