CAG aeleza jinsi ATCL ilivyopata hasara ya Sh150 bilioni

CAG aeleza jinsi ATCL ilivyopata hasara ya Sh150 bilioni

Muktasari:

  • Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeeleza kuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limepata hasara ya Sh150 bilioni katika kipindi cha miaka mitano.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeeleza kuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limepata hasara ya Sh150 bilioni katika kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza leo Alhamisi Aprili 8, 2021 katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma CAG, Charles Kichere amesema, “mwaka huu imetengeneza hasara ya Sh60 bilioni na kwa miaka mitano imetengeneza hasara ya takribani Sh150 bilioni.”

Hata hivyo, Kichere amesema wamebaini  changamoto zinazotakiwa kushughulikiwa na Serikali ili kuimarisha utendaji katika shirika hilo, “nilibaini bodi ya wakurugenzi haina mjumbe hata mmoja mwenye uzoefu kwenye mambo ya usafiri wa anga.”

“Wakati wa changamoto ya corona ndege nyingi zilikuwa zimesimama lakini ATCL ilikuwa inatozwa gharama za ukodishwaji bila kujali ndege zilikuwa hazifanyi kazi kutokana na changamoto ya Covid 19. Hii inatokana na kwamba mkataba wa ukodishaji kati ya TGFA na ATCL hauna kipengele ‘kama haifanyi kazi tusilipe’.”

Amesema kati ya Machi hadi Juni 2020, ATCL ilitozwa Sh15.4 bilioni kwa ajili ya ukodishaji wa ndege wakati zilikuwa hazitoi huduma na pia shirika hilo limerithi madeni makubwa na riba.

“Kwa miaka mitano ilikuwa Sh45 bilioni na mwaka wa fedha 2019/20 imetozwa riba ya Sh12.4 bilioni. Ndege za ATCL kusafiri kwenda nje ya nchi zinaweza kukamatwa huo ni ukweli. Pia kuna changamoto ya viwanja vya ndege nchi ndege za ATCL haziwezi kuruka usiku.”

“Na baadhi ya viwanja haziwezi kutua zikiwa zimechukua abiria kwa uwezo wake, mfano uwanja wa ndege wa Dodoma Airbus haiwezi kutua ikiwa na abiria 162 maana uwezo wa uwanja huo kuhimili ndege hiyo kutua ikiwa na idadi hiyo ya watu haupo,” amesema.

Katika ufafanuzi wake amesema, “tulifanya ukaguzi wa kiutendaji ATCL na kubaini yafuatayo,  hadi kufikia Juni 30 Serikali ilikuwa imenunua ndege nane kwa Sh1.2 trilioni katika juhudi za kufufua kampuni ya ndege.”

"Ndege hizo zinamilikiwa na wakala wa ndege za Serikali na ATCL inazikodisha. Pamoja na kununua ndege hizo kwa miaka mitano 2015/2020 Serikali imeisaidia kiasi cha Sh153 bilioni kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na maendeleo.”