CAG: Sh18 bilioni zilizokusanywa wilaya 135 nchini hazikufikishwa benki

Thursday April 08 2021
wasafipic

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ripoti za mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha mapato ya Sh18.769 bilioni yaliyokusanywa katika halmashauri za Wilaya 135 hayakufikishwa benki.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 8, 2021 na CAG,  Charles Kichere wakati akisoma ripoti zinazoishia Juni 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma.

“Nilipitia taarifa za makusanyo za mamlaka za Serikali za mitaa 135 na kubaini kuwa Sh18.769 bilioni  zilikusanywa kutoka vyanzo mbalimbali, hata hivyo hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa kiasi hicho kiliwasilishwa benki,” amesema Kichere.

Amesema hiyo inaashiria usimamizi hafifu wa mapato katika halmashauri za wilaya nchini.

“Kutopatikana kwa nyaraka zinazoonyesha mapato yaliyokusanywa yalipelekwa benki kulinizuia kujiridhisha kuhusu uhalali, usahihi na ukamilifu wa kiasi cha mapato kilichokusanywa na kuwekwa kwenye taarifa za fedha za halmashauri husika,” amesema CAG Kichere.

Advertisement