CCM yalishukia gazeti la Uhuru
Muktasari:
- Chama hicho tawala kimechukizwa na habari inayohusu Rais Samia Suluhu Hassan kugombea urais mwaka 2025.
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimechukizwa na habari iliyoandikwa na gazeti lake la Uhuru inayohusu Rais Samia Suluhu Hassan kugombea urais mwaka 2025 iliyotokana na mahojiano ya kiongozi huyo na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka imesema habari hiyo yenye kichwa ‘Sina wazo kugombea urais 2025- Samia’ imepotosha na kwamba chama hicho kitawachukulia hatua za kinidhamu wote waliohusika katika uandaaji wa habari hiyo.
“Rais Samia Suluhu Hassan hakusema kabisa maneno hayo, hili ni kosa kubwa linalokwenda kinyume na sera inayoongoza vyombo vya habari jambo ambalo halitavumiliwa hata kidogo hivyo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika katika uandaaji wake.
Soma hapa: Rais Samia azungumzia kesi ya Mbowe
“Gazeti la Uhuru ndio ‘Adam na Hawa’ wa magazeti yote hapa nchini linawajibika kuonyesha weledi wa hali ya juu na sio vinginevyo.
“Tunawaomba wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Watanzania kwa ujumla kupuua habari hiyo kwani imeandikwa na watu wenye maslahi yao binafsi,” imesema taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa fikra na nguvu za Rais Samia zimejikita katika kuwatumikia Watanzania na si vinginevyo.