CCM yataka utatuzi changamoto mipaka ya shule

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Morogoro mjini, Fikiri Juma (kulia) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Ally Machela(wa pili kutoka kulia). Kushoto ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlimani. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Kukosekana kwa uzio na alama za kudumu za mipaka kwenye shule nyingi, Manispaa ya Morogoro, kumesababisha wananchi kuvamia maeneo hayo huku wakiyageuza kuwa sehemu za biashara na makazi.
Morogoro. Kukosekana kwa uzio na alama za kudumu za mipaka kwenye shule nyingi, Manispaa ya Morogoro, kumesababisha wananchi kuvamia maeneo hayo huku wakiyageuza kuwa sehemu za biashara na makazi.
Hali hiyo pia inaelezwa kuchangia wanafunzi kutoroka kwa kuwa Hapana kizuizi cha aina yeyote.
Hii ndiyo sababu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma pamoja na kamati yake ya siasa wilaya hiyo, wamemuelekeza uongozi wa manispaa na shule hizo, kuangalia namna bora ya kumaliza changamoto hizo.
Rai hiyo imetolewa leo Jumamosi 7, 2023 wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo inahusisha Kituo cha Afya Tungi, Zahanati, Shule ya Sekondari Boma, Lukobe na ujenzi wa ofisi za kata.
Pia kamati hiyo imekagua miradi ya maji, umeme, barabara pamoja na mifumo ya ukusanyaji mapato ya halmashauri hiyo na hasa katika vituo vya mabasi.
Mwenyekiti huyo amesema wapo wadau wa maendeleo wa ndani ambao wana moyo na kusaidia hiyo amewataka viongozi hao kuwaalika katika vikao na kuwaeleza changamoto ili ufumbuzi upatikane.
"Kikubwa niwasihi, hawa wadau msiwaombe pesa, wekeni mikakati na mipango kazi yenu vizuri waitieni kwenye vikao muwaeleze changamoto halafu waombeni vifaa, kama mnachangamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo basi waombeni wawape tofali, saruji, mchanga, bati na vifaa vingine badala ya kukimbilia kuomba fedha," amesema Juma.
Aidha katika ziara hiyo kamati imegundua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa halmashauri, wakiwemo walimu wenye malalamiko ya juu ya kupandishwa na madaraja lakini pia na stahiki zao.
Vilevile kumekuwepo mwamko mdogo wa wazazi na walezi katika kuchangia fedha za chakula cha mchana kwaajili ya wanafunzi jambo ambalo linadaiwa ama kuongeza utoro au kusababisha wanafunzi kushindwa kuelewa masomo yako kutokana na njaa.
Hivyo basi, Mwenyekiti Juma amewataka wazazi na walezi kuanza kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao ili waweze kuwa na utulivu wanapokuwa shuleni, huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ally Machela, kutuma timu ya wataalamu watakaopima maeneo ya shule zenye migogoro ya mipaka na kuweka uzio.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo amewataka walimu wenye malalamiko ya kutopandishwa madaraja, kutolipwa fedha za likizo kuwasilisha kwa maandishi malalamiko hayo ofisini kwake ili yaweze kufanyiwa kazi.
Kuhusu changamoto ya uchakavu na uhaba wa matundu ya vyoo mkurugenzi huyo ameahidi kutatua changamoto hiyo haraka kabla ya wanafunzi wa darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza hawajaanza masomo mwezi Januari 2024.
Baadhi ya madiwani wameishukuru kamati hiyo Kwa kutembelea miradi na kuona changamoto zilizopo kwenye kata zao, wakiamini ziara hiyo itawezesha kutatuliwa kwa changamoto hizo.
Pascal Kihanga, Diwani wa Kata ya Mazimbu ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Morogoro, amesema kupitia Baraza la Madiwani, atakahikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa kuwa bajeti ilishatengwa.
"Tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha nyingi za kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo madarasa, sisi kama madiwani tutahakikisha fedha hizo zinakwenda kumaliza miradi iliyokusudiwa," amesema Kihanga.