CDF Mabeyo: Vyombo vya ulinzi na usalama vitamtii Rais Samia

CDF Mabeyo: Vyombo vya ulinzi na usalama vitamtii Rais Samia

Muktasari:

Mkuu wa Majeshi  nchini Tanzania (CDF) Venance Mabeyo amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitamtii na kutekeleza majukumu yake kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi  nchini Tanzania (CDF) Venance Mabeyo amemhakikishia Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitamtii na kutekeleza majukumu yake kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema vyombo hivyo vitaendelea kuonyesha uadilifu, utiifu na uaminifu kwake kama ilivyokuwa kwa awamu za uongozi zilizopita.

Akizungumza katika ibada ya mazishi ya Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Magufuli leo Ijumaa Machi 26, 2021 wilayani Chato Mkoa wa Geita kwa niaba ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama,  Mabeyo ameeleza kuwa hali ya nchi ni shwari na wataendelea kuimarisha ulinzi.

“Ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vyombo vitaendelea kukulinda kama rais, kukutii kama amiri jeshi mkuu na kutekeleza majukumu yetu kama ilivyoainishwa kwenye katiba.”

“Vyombo vya ulinzi na usalama vinakuhakikishia utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kama ilivyo mila na desturi kwa majeshi yetu katika awamu zote zilizopita,” amesema.

Mabeyo ametumia fursa hiyo kumualika Rais Samia kuwatunuku nishani askari wanafunzi waliotakiwa kutunikiwa nishani hizo Machi 10, 2021.

“Hayati Magufuli alitakiwa awatunuku  nishani Februari 20 lakini kutokana na kazi zake tukasogeza mbele hadi Machi 6...,alipomaliza ziara yake Dar es Salaam akaniambia hajisikii vizuri hivyo akaomba tusogeze hadi Machi 10 ili ajitazamie afya yake,” amesema.

Akimzungumzia Magufuli amesema tangu  aingie madarakani mwaka 2015  alionyesha kuviamini na kuvipenda vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuviwezesha

kwa mahitaji ya kiutendaji na kiutawala ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Alionyesha pia kwa namna alivyovishirikisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo ya nchi. Katika hali hiyo vyombo vyetu vilishirikishwa katika shughuli zote za kiuchumi mfano kujenga na kuulinda ukuta wa mgodi wa Tanzanite.”

“Katika kipindi alichoongoza taifa alijikita katika kujenga uchumi ambako aliwekeza kwenye miradi ya kimkakati na kuweka miundombinu bora,” amesema Mabeyo.