Chadema kuendelea kutumia ibada kumuombea Mbowe, kudai Katiba Mpya

Wanachama wa Chadema baada ya kumaliza ibada ya kumuombea Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe na kudai Katiba mpya katika Kanisa Katoliki Epiphania ya Bugando jijini Mwanza leo. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea na mbinu yao mpya ya kudai Katiba Mpya kwa kwa njia ya amani kwa kutumia ibada zinazoendeshwa katika makanisa mbalimbali jijini Mwanza.

Mwanza. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea na mbinu yao mpya ya kudai Katiba Mpya kwa kwa njia ya amani kwa kutumia ibada zinazoendeshwa katika makanisa mbalimbali jijini Mwanza.

Chama hicho pia kinatumia ibada hizo kumuombea mwenyekiti wao taifa, Freeman Mbowe anayekabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kwa kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Hiyo ni baada ya viongozi na wanachama wa chama hicho mkoa wa Mwanza kuhudhuria ibada na kufanya maombi katika Kanisa Katoliki Epiphania ya Bugando lililoko katikati ya jiji hilo.

Akizungumza na Mwananchi Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema mbinu hiyo imeonyesha ufanisi huku mwitikio kwa wanachama wa chama hicho kuhudhuria ibada hizo ukiongezeka.

"Leo idadi ya wanachama wa Chadema waliohudhuria maombi ya kumuombea Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe na kudai Katiba Mpya imeongezeka kuna waliovalia sare za chama na ambao hawakuvaa sare za chama," amesema Obadi.

Ameongeza kwamba chama hicho kitaendelea kudai Katiba Mpya katika maeneo yenye mikusanyiko na kwenye nyumba za ibada bila hofu huku wakiamini kwamba Mungu atafanya muujiza wake ili kufanikisha jambo hilo.

"Tunamuombea na Rais Samia Suluhu Hassan ili Mungu amshushie hekima ili aweze kuona ulazima wa kuwa na Katiba Mpya na tunaamini tutaipata," amesisitiza Obadi.

Chadema kuendelea na ibada kumuombea Mbowe

Obadi ameongeza; "Nitoe wito kwa wanachama wa Chadema Kanda ya Victoria kuondoa hofu, waje wajiunge nasi kumuombea mwenyekiti wetu na kudai Katiba Mpya kwa njia ya amani,"

Zaidi ya wanachama 50 waliokuwa wamevaa sare za Chadema na skafu wameonekana katika misa hiyo iliyohitimishwa saa 3:30 asubuhi ya leo.