Chande: Tumemalizana na Zanzibar deni la Umeme

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande amesema wamemaliza migogoro na Shirika la Umeme la Zanzibar (Zesco) baada ya kukaa na kukubaliana viwango vya tozo za umeme.

Chande amebainisha hayo leo Mei 26, 2023 wakati akijibu maswali ya wahariri wa vyombo vya habari katika majadiliano yaliyofanyika kujadili sekta hiyo ya umeme.

Mkurugenzi alikuwa akijibu swali la mwanahabari mkongwe, Salim Salim aliyetaka kujua deni ambalo Tanesco inaidai Zesco la Sh65 bilioni zimefikia wapi hadi sasa.

Chande amesema suala hilo la deni limemalizika na kwamba huko nyuma hawakuwa na makubaliano ya viwango vya tozo ya umeme, kila upande ulikuwa ukisimamia upande wake.

"Tulikuwa na tariff (tozo) mpya, sasa tunakwenda vizuri. Tumekaa tumezungumza na tumekubaliana na yale madeni ya nyuma tumeyamaliza," amesema Chande.

Ameongeza kwamba wamefanya upembuzi na kuongeza cable tatu zitakazomwenda Zanzibar kwa sababu shughuli za kiuchumi zimeongezeka.

"Kwa sasa hatuna ugomvi katika hilo, tumeliweka vizuri," amesema Chande wakati akijibu maswali mbalimbali ya wahariri wa vyombo vya habari nchini.