Chanjo ya majaribio ya Ukimwi kukamilika Juni 2024

Mkurugenzi Mtendaji wa Hosptali y Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) Dk ,Godlove Mbwanji ,akizungumza kwenye kongamano ya kisayansi, kitaaluma na tafiti  (Share) katika Ukumbi wa Hotel ya Eden Jijini Mbeya Leo. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr),  Profesa Said Abood  amesema leo Alhamisi Septemba 21, 2023 kwenye Kongamano la Kisayansi, Kitaaluma na Tafiti (Share) lililohususha  wanasayansi 250 kutoka Tanzania na  Afrika Mashariki, Kenya, Uganda na Nigeria.

Mbeya. Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) imesema inatarajia kutoa matokeo ya awamu ya pili ya chanjo ya majaribio ya  maambukizi mapya  ya virusi vya  Ukimwi mapema  mwezi Juni 2024.

Imeelezwa kuwa utafiti wa chanjo hiyo  ulianza kufanywa mwaka 2018 katika vituo viwili nchini kikiwepo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Mkoa wa Mbeya na Chuo Kikuu Cha Sayansi Shirikishi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Moi).

Mkurugenzi Mkuu wa Nimr,  Profesa Said Abood amesema leo Alhamisi ,Septemba 2023 Mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi, Kitaaluma na Tafiti (Share,) lililifanyika katika ukumbi wa Hotel ya Eden na kushirikisha wanasayansi 250 kutoka maeneo mbali mbali nchini ikiwepo ,Kenya ,Uganda na Nigeria.

Profesa Abood amesema tafiti za chanjo ziko katika awamu tatu ambapo kwa sasa iko katika hatua  ya  pili ambayo ilianza kufanywa mwaka 2018 na inakamilika  Juni 2024 ambayo kimsingi italeta matokeo mazuri na kuifanya Tanzania kutotegemea dawa kinga kutoka mataifa mengine nchini.

“Tunataka kuboresha huduma  za afya  kwa wananchi kwani maendeleo tafiti wa  chanjo ya majaribio uko katika   hatua nzuri kwa sasa tunaangalia uwezo wa kuhudumia wagonjwa ambao wako kwenye hatari ya juu ya maambukizi  mapya ya VVU  kwa kupata chanjo na dawa kinga,”amesema.

Ameongeza kuwa “Tunaendelea na tafiti za kisayansi  ya  chanjo  kuona uwezo wake akipewa mtu mwenye hatari ya juu ya maambukizi  mapya ya VVU, lengo ni kuona Tanzania inazalisha dawa tiba na siyo kutegemea kutoka mataifa ya nje,”amesema.

Kongamano hilo la siku mbili lengo  kuu ni  kubadilishana uzoefu wa tafiti za kisayansi na afya kwa kujadiliana ili kuleta tofauti ya mabadiliko ya kisera na   kusaidia Serikali kufanya maamuzi mbalimbali ya  kuboresha   huduma kwa wananchi.

Akifungua kongamano hilo,

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali,  Dk Nyembea Hamad amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya na kuweka  kipaumbele cha  kusaidia upatikanaji wa taarifa za tafiti na kisayansi ambazo zitaleta matokeo mazuri kwa wadau.

“Kwa muda wa Siku mbili za kongamano hilo tunatarajia kutoka na matokeo mazuri kwa kupeana uzoefu ambao utakuwa chachu za kuboresha huduma katika vituo vya afya na kuondoa kero kwa wananchi  kwa kuzingatia taarifa za kitafiti,”amesema.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika  HJMRI, Dk Magnus Ndolichimpa amesema kupitia  kongamano hilo wanatarajia litaleta matokeo mazuri ya tafiti ya kisayansi zitakazosaidia kuboresha miradi ya Ukimwi na kifua kikuu.

“Tumekutana na wadau wa kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali nchini  lengo ni kuona  tunakwenda kuboresha huduma kwa pamoja kwa Watanzania,”amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda (MZRH), Godlove Mbwanji amesema tafiti zitakazojadiliwa zitaleta tija kubwa katika utoaji huduma kwa watu walio katika hatari ya kupata magonjwa ya Ukimwi na kifua Kikuu.

Mshiriki katika kongamano hilo kutoka Taasisi ya Mama Afrika (Samofa), Thabitha Bughali amesema kuwa elimu inayotolewa kupitia kongamano hilo ifikishwe kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu ili kufanikisha upatikanaji wa tafiti za wagonjwa wa VVU na Ukimwi.