Chongolo awataka wagombea kusuka ama kunyoa

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo emeelekeza viongozi wote wa chama hicho nchini, wanaowania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa ndani, kuachia nafasi zao ili wasiwe sehemu ya usimamizi.

Shinyanga. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo emeelekeza viongozi wote wa chama hicho nchini, wanaowania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa ndani, kuachia nafasi zao ili wasiwe sehemu ya wasimamizi wa uchaguzi huo.

Kauli hiyo ya Chongolo inakuja baada ya kile alichokisema kuwa kumeonekana changamoto hiyo katika uchaguzi wa ndani wa CCM katika ngazi ya mashina.

"Natoa agizo, kumekuwa na kamchezo na tumeona katika uchaguzi ngazi ya mashina, unakuta Katibu wa Kata anagombea au wa Tawi anagombea alafu yeye mwenyewe ndiyo anatoa fomu inawezekanaje, haki itapatikanaje," alisema.

Katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani Shinyanga jana, Chongolo leo Mei 27, 2022 amewaagiza viongozi wanaogombea nafasi hizo kukaa pembeni, badala yake uongozi wa juu uteue wengine kusimamia mchakato huo.

Kwa mujibu wa Mtendaji huyo Mkuu wa chama hicho, kufanya hivyo kutafanikisha utendaji haki kwa wagombea wote wa uongozi ndani ya CCM.

"Kuanzia leo nchi nzima, mahali ambapo pana kiongozi anayegombea, kiongozi huyo atakaa pembeni asishiriki kikao cha maamuzi ili awatendee haki wenziwe na wenziwe wamtendee haki yeye," alisema.

Kinyume na kufanya hivyo, alisema ujanja ujanja wa kuficha fomu na kupitisha viongozi wasio na sifa hautaisha.

Pia, aliwawaonya viongozi waliopewa dhamana na chama hicho, kuacha kueneza fitina na majungu dhidi ya wengine wakati wa uchaguzi wa ndani.

"Tatizo lililopo ni baadhi ya wanaopewa dhamana kwenye maeneo kutokutenda haki. Marufuku kwa yeyote kuineza fitina, majungu, uongo na uzushi dhidi ya wengine wakati wa uchaguzi," alisema.

Amewataka kutenda haki, akieleza kuwa haiwezekani wakati wote tangu mwaka 2017 viongozi hao wamekuwa ndani ya CCM lakini hawakuwahi kuonywa wala kujadiliwa kwenye vikao vya maadili, iweje tuhuma hizo ziibuke sasa.

"Kwenye kikao cha maadili haitwi, kwenye kikao cha kuulizwa haitwi, kwenye kikao cha kuhojiwa haitwi, mmefika wakati wa uchaguzi vikao asubuhi mchana jioni. Ooh... huyu mbaya, huyu mlevi, huyu mfupi, huyu mnene, anakuhusu nini?" alihoji.

Kuhusu zao la Pamba, amewaagiza wakulima kuhakikisha wanazalisha kwa ubora ili kutengeneza tija na kuwa na ushindani katika soko.

Amesema zao hilo mwaka huu litauzwa Sh1,562 ambayo ni zaidi ya ile ya mwaka jana, ambayo ni Sh1,050.

Katibu wa Halmashauri Kuu, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga, amezungumzia changamoto ya kupanda kwa bei ya bidhaa akisema inatokana na changamoto za ulimwengu.

"Ndugu zangu bidhaa zimepanda bei kutokana na janga la Corona na vita ya Urusi na Ukraine, Serikali imejitahidi kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni kuleta ahueni ya bei ya mafuta, hii inaonyesha tunawajali," alisema.