Chuo Kikuu cha Aga Khan chaingia makubaliano na Tawiri
Muktasari:
- Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini, chaingia makubaliano na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) ili kukuza maendeleo ya utafiti na kubadilishana uzoefu.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) nchini, kimesaini mkataba wa makubaliano na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri), unaolenga kunufaisha maendeleo ya tafiti na uandaaji sahihi wa sera.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Februari 22, 2023 na AKU, imeeleza kuwa ushirikiano utaziinua taasisi hizo hasa Chuo Kikuu cha Aga Khan, tawi la Arusha katika kufanya tafiti za wanyamapori, ikiwemo uchavushaji, ufugaji wa nyuki na utafiti wa nyuki kwa ajili ya kuboresha maisha na uhifadhi wa mazingira.
“Tutakuwa tukibadilishana uzoefu kutoka Tawiri kwenda AKU na AKU kwenda Tawiri ili kuwezesha watafiti kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya uhifadhi na kuandika matokeo ya utafiti.
“Tunatarajia kuwapeleka wanafunzi wetu baadaye katika taasisi ya Tawiri ili kujifunza zaidi kuhusu kazi zinazoendelea hatua na mbinu ya utafiti,” amesema Dk Carl Amrhein, ambaye ni Makamu Mkuu wa AKU.
Dk Amrhein amesema kwa sasa AKU infanya kazi na Tawiri kutekeleza miradi ya utafiti kuhusu uchavushaji na jukumu lao katika kukuza kilimo endelevu nchini Tanzania.
"Tumekuwa tukifanya kazi na washirika wengine wengi kutekeleza miradi mbalimbali ya utafiti - miradi ya kitaifa na kimataifa. Kwa sasa, Tawiri inasimamia zaidi ya miradi 20 ya utafiti katika maeneo mbalimbali.
“Kupitia utafiti, Tawiri imechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii na maisha miongoni mwa jamii hasa zile zinazopakana na maeneo ya hifadhi,” amesema Dk Eblate Mjingo, Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri.