Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chura anayeishi juu zaidi Afrika agunduliwa Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

  • Chura aina ya Amietia wittei, sasa anageuka kuwa ishara ya matumaini, wito wa uhifadhi, na ushahidi hai wa uimara wa maisha katika mazingira magumu kabisa.

Moshi. Katika kile kinachotajwa kuwa ugunduzi wa kihistoria, chura mdogo wa ajabu amebainika kuishi katika mazingira magumu ya Mlima Kilimanjaro, kwenye urefu wa mita 3,960 kutoka usawa wa bahari na kumfanya kuwa chura anayeishi juu zaidi barani Afrika kuwahi kurekodiwa.

Chura huyo wa aina ya Amietia wittei, anayejulikana kama Chura wa Mtoni wa Witte, alionekana kwa mara ya kwanza na kundi la wapanda mlima kutoka kampuni ya Altezza Travel mnamo Juni 2024, wakiwa katika safari ya kuelekea kilele cha mlima huo maarufu duniani. 

Kutokana na ugunduzi huo usiotarajiwa, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) iliungana na kampuni hiyo kufanya utafiti maalum kuthibitisha uwepo wake.

Timu ya wataalamu, ikiwemo mtafiti mashuhuri wa amfibia kutoka Afrika Kusini, Profesa Alan Channing, ilifanya utafiti katika vijito vya mwinuko kati ya mita 3,600 hadi 4,100. 

Wataalamu hao waligundua makundi kadhaa ya vyura hao wakiwa wanaishi kwenye mazingira yenye baridi kali, kiwango kidogo cha oksijeni na hatari kubwa za asili, hali inayowafanya kuwa wa kipekee zaidi kuliko spishi nyingine yoyote ya chura barani Afrika.

Kabla ya ugunduzi huu, vyura wachache sana walishawahi kurekodiwa wakiishi juu ya mita 4,000 duniani kote, na hakuna hata mmoja aliyewahi kupatikana Afrika. Spishi hii imevunja dhana ya muda mrefu kuwa mazingira ya juu ya Kilimanjaro hayawezi kuhimili maisha ya amfibia kama vyura.

“Ni kama kugundua uhai kwenye sayari nyingine,” alisema Profesa Channing. “Maeneo haya yana baridi kali, hewa nyepesi na miinuko mikali, lakini bado chura huyu anaishi hapa.”


Tishio kutokana na binadamu, tabianchi 

Pamoja na mafanikio ya ugunduzi huo, wataalamu wameeleza wasiwasi juu ya hatari zinazoikabili spishi hiyo adimu. Uchafuzi wa maji kutokana na shughuli za utalii, hususan uoshaji wa vyombo kwa sabuni, umebainika kuathiri moja kwa moja makazi ya vyura hao.

Vilevile, mabadiliko ya tabianchi yamesababisha baadhi ya vijito kukauka kabisa wakati wa kiangazi, hali inayotishia uwezo wao wa kuzaa na kuendelea kuishi.

“Katika vijito vilivyokuwa na athari za sabuni, hatukuona hata kiluwiluwi mmoja,” alisema Wilirk Ngalason Mroso, mtafiti kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam. “Ni dhahiri kuwa hata kiasi kidogo cha uchafuzi kinaathiri bioanuwai ya maeneo haya.”


Ulinzi wake 

Kwa bahati nzuri, chura huyo anaishi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, jambo linalompa ulinzi wa kisheria dhidi ya uharibifu wa mazingira. Hata hivyo, wataalamu wanasema hatua za dharura zinahitajika, ikiwemo kuimarisha udhibiti wa shughuli za utalii na kuhamasisha matumizi rafiki kwa mazingira.

Peter Lyamuya, mmoja wa viongozi wa msafara wa utafiti huo, alisema: “Chura huyu anaweza kuwa mdogo kwa mwonekano, lakini ujumbe wake ni mkubwa. Ni kengele ya tahadhari kwamba tuna wajibu wa kulinda mazingira haya nyeti kwa maslahi ya viumbe wote wakiwemo binadamu.”


Fundisho kwa dunia 

Ugunduzi huu unaelezwa kuwa ni ukumbusho mkubwa kuwa sayari yetu bado ina mafumbo mengi yasiyojulikana, hata katika maeneo kama Kilimanjaro ambayo huchukuliwa kuwa yamechunguzwa vya kutosha. 

Chura huyu wa mlimani sasa anageuka kuwa ishara ya matumaini, wito wa uhifadhi, na ushahidi hai wa uimara wa maisha katika mazingira magumu kabisa.

Hata hivyo, kampuni ya Altezza Travel imetoa shukrani kwa TAWIRI, TANAPA na Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro kwa kushirikino wao katika kufanikisha utafiti huo.