CRDB, ATCL waungana kwenye mfumo wa malipo

Tuesday December 14 2021
CRDB PIC

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Denge la Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi wakionyesha ishara ya uzinduzi wa huduma ya malipo ya tiketi za ndege za ATCL kupitia mtandao wa Benki ya CRDB unaojumuisha matawi, CRDB Wakala na SimBanking katika hafla iliyofanyika leo jijini Arusha katika hoteli ya Mount Meru.

By Mwandishi Wetu

Arusha. Benki ya CRDB imeingia ubia na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa kuunganisha mfumo wa malipo ili kuwawezesha wateja wa shirika hilo kulipia tiketi zao kupitia benki hiyo yenye mtandao mkubwa nchini.

Baada ya ubia huo wateja wa ATCL popote walipo wataweza kulipia tiketi zao za safari kwa kutumia matawi 268 yanayopatikana nchi nzima, CRDB Wakala zaidi ya 20,000 pamoja na huduma ya SimBanking inayowezesha kufanya malipo kidijitali.

Akizungumzia ubia huo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema utasaidia kuhakikisha wateja wanafanya malipo kwa urahisi popote pale walipo nchini jambo ambalo alilieleza kuwa litasaidia kuboresha huduma kwa wateja katika shirika hilo.

“Pamoja na kuwa wateja watakuwa wakilipia tiketi zao kwa urahisi, vilevile uunganishwaji wa mfumo huu wa malipo na mfumo wa ATCL utasaidia kuongeza ufanisi katika upande wa upokeaji wa malipo ya tiketi,” alisema Nsekela.

Nsekela alibainisha kuwa awali wateja walikuwa wanaweza kulipia tiketi za ndege za ATCL kwa njia ya mtandao kupitia TemboCard pekee hivyo kuongezeka kwa njia hizo nyengine kunawapa wateja uhuru wa kufanya malipo kwa njia ambayo ni rahisi kwao kwa wakati husika.

Mkurungezi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema ubia huo wa kibiashara wa kuunganishwa kwa mifumo ya malipo ya Benki ya CRDB kunaendana na mikakati ya ukuaji wa shirika hilo ambapo hivi karibuni limeongeza safari za ndege ndani na nje ya nchi.

Advertisement

“Mkakati wa upanuzi wa biashara unaenda sambamba na kuhakikisha wateja wetu wanaweza kupata huduma bora popote pale walipo. Ni imani ushirikiano huu na Benki ya CRDB utasaidia kufikia azma yetu ya kutoa huduma bora za usafiri kwa njia ya anga,” alisema Matindi.

Hivi karibuni ATCL limeongeza safari zake za ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni kipindi kifupi baada ya ujio wa ndege mpya mbili aina ya Airbus, ambazo zimepelekea kuongezeka kwa safari mpya zilizoanza Novemba, 2021.

Safari zilizoongezwa ni pamoja na Dodoma-Mwanza, Dar-Mtwara, Dar-Nairobi, Dar-Ndola Dar-Bujumbura ambapo Benki ya CRDB ina kampuni tanzu, pamoja na Dar-Lumbumbashi ambapo Benki hiyo ipo mbioni kufungua kampuni tanzu.

Advertisement