CUF yapata pigo jingine

Makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu akimkabidhi kadi ya uanachama aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wanawake CUF (Juke), Kiiza Mayeye leo Jumanne Mei 23, 2023

Muktasari:

  • Chama cha Wananchi (CUF) kimepata pigo baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake (JUKE), Kiiza Mayeye kujiunga na Chama cha cha ACT Wazalendo.

Dar es Salaam.  Chama cha Wananchi (CUF) kimeeendelea kupata pigo baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake (JUKE), Kiiza Mayeye kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo.

Hivi karibuni mamia ya wanachama waliondoka kwenye chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaadema).

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Doroth Semu, Kiiza amesema amefanya uamuzi huo ili kuendeleza mapambano.

 "Nimefanya uchambuzi wa kina na kujiridhisha kuwa ACT Wazalendo ndio jahazi sahihi la kuendeleza harakati zangu kwa ajili ya kuwakomboa wanachi wa Kigoma Kaskazini na Mkoa mzima wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla," ammesema Kiiza.

Kiiza ambaye pia amewaahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CUF 2015 hadi 2020 na mgombea ubunge katika uchaguzi Kigoma Kaskazini, amesema amejiunga na chama hicho ili kuongeza nguvu kwenye ujenzi wa chama katika kujihakikishia ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

 "Leo, nimelazimika kuchukua maamuzi haya magumu kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika, mimi ni mwanasiasa wa vitendo naamini siasa halisi ipo chini (field) kwa wananchi,"

 "Mwaka 2020 niligombea ubunge katika jimbo la Kigoma Kaskazini na kwa matokeo halisi nilishinda lakini, kilichotokea unakifahamu,"amesema.

Aidha Kiiza amesema ameshawishika pia na jitihada za ACT Wazalendo kuimarisha mtandao wake nchi nzima na jitihada za chama hicho kukuza vipaji vya vijana na wanawake.

"Kabla sijafanya uamuzi huu nimezungumza na vyama vingi ili kufanya utafiti kabla ya kujiunga na Chama husika, mwishowe nikafanya hitimisho kuwa ACT Wazalendo ndio jukwaa sahihi" amesema.

Hata hivyo Kiiza amesema anatarajia kwenda Kigoma Kaskazini hivi karibuni huko ataeleza kwa kina zaidi kwa nini chama hicho hiki kinapaswa kuwa tumaini lao kutokana na utafiti na uchambuzi wa kina alioufanya.