CWT: Ujenzi vyumba vya madarasa utapunguza msongamano wa wanafunzi

Muktasari:

  • Jumla ya madarasa 15,000 yamejengwa na serikali nchi nzima kutokana na fedha za mkopo kiasi cha Sh1.3 trilioni ambazo serikali ilizipokea kutoka Shirika la Fedha duniani (IMF). Madarasa hayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi.

Dar es Salaam. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Morogoro kimesema ujenzi wa vyumba vya madarasa nchi nzima uliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan utasaidia kupungunza msongamano wa wanafunzi madarasani na kurahisisha ufundishaji kwa walimu.

Hayo yamebainishwa leo Januari 14, 2021 jijini Dar es Salaam na mwenyekiti wa CWT mkoa wa Morogoro, Jumanne Nyakirangani wakati akimpongeza Rais Samia mbele ya waandishi wa habari kutokana na ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa nchini.

Amesema uwepo wa vyumba hivyo vya madarasa hasa katika mkoa wa Morogoro utasaidia pia walimu kuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na kuwepo kwa utulivu wa wanafunzi darasani.

“Ni wazi kuwa utulivu utapatikana kwa wanafunzi kwani zamani unakuta darasa moja ilikuwa na wanafunzi zaidi ya 150, hali ambayo ilikuwa inapoteza utulivu kwa walimu. Kwa hiyo vyumba hivi vitasaidia kuwa na wanafunzi wachache mwisho 40 na walimu kufundisha wakiwa na amani,” amesema Nyakirangani.

Nyakirangani amewaomba wazazi kujitokeza kwa wingi kuwaandikisha watoto wao ili waweze kupata elimu bora itakayowafaa maishani.

“Niwaombe wazazi, jitokezeni kwa wingi kuwapeleka watoto shule, mazingira yaliyoandaliwa na Rais Samia ni mazuri mnoo, msirudi nyuma endeleeni kuiunga mkono Serikali kwa kuwapeleka watoto shule,” amesema mwenyekiti huyo.

Vilevile, amempongeza Rais Samia kwa kusikiliza madai yao ya kupandishwa madaraja na maslahi mengine ambayo wameahidiwa kuwa yatafanyiwa kazi kwa wakati.

“Mwaka jana zaidi ya watumishi 100,000 walipandishwa vyeo, wengi wao walikuwa ni walimu. Pia, walimu wanaendelea kupandishwa madaraja na viongozi wameshapatiwa mafunzo na sasa tunakwenda kutoa hayo mafunzo kwa wanachama, hivyo niendelee kuwaomba walimu waendelee kuwa watulivu,” amesema.