Daktari aliyeingia nchini kumwona mke wake apigwa faini ya Sh1milioni

Daktari aliyeingia nchini kumwona mke wake apigwa faini ya Sh1milioni

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia wawili wa Rwanda, kulipa faini ya jumla ya Sh1.5milioni au kwenda jela miaka miwili, akiwemo Dk Ally Rugaravu aliyekuja nchini kumsalimia mkewe bila kuwa na kibali na kughushi vibali vya kazi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia wawili wa Rwanda, kulipa faini ya jumla ya Sh1.5milioni au kwenda jela miaka miwili, baada ya kupatikana na hatia katika makosa matatu, ambayo ni kuwepo nchini bila kuwa na kibali na kughushi vibali vya kazi.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Dk Ally Rugaravu (41) na mwanafunzi Abduljalil Munyakazi (21), wote kutoka nchini Rwanda, ambao walikuwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 180/2021.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Oktoba 12, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi, baada ya washtakiwa kukiri mashtaka yao.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Simba, amesema washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa

"Mshtakiwa Rugaravu, umetiwa hatiani kwa makosa yako mawili, hivyo shtaka la kwanza ambalo ni kukutwa nchini bila kuwa na kibali, Mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela mwaka mmoja.

“Shtaka la pili ambalo ni kughushi kibali cha makazi, Mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh 500,000 na ukishindwa utatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela," amesema Hakimu Shaidi.

Hakimu Shaidi amesema kwa mshtakiwa pili katika kesi hiyo, Muyakazi yeye ametiwa hatiani katika kosa moja la kughushi kibali cha makazi, hivyo atatakiwa kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela mwaka mmoja.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Sitta Shija akisaidiana na Godfrey Ngwijo, waliomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hivyo.

Pia, kabla ya kutoa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa washtakiwa hao kujitetea kwanini wasipewe adhabu Kali.

Mshtakiwa Dk Rugaravu aliomba kupunguziwa adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na alikuja nchini kumuangalia mke wake.

Katika kesi ya msingi, wakili Shija amedai kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao, Oktoba 6, 2021, eneo la Magomeni, Watumishi Housing kitalu namba A02.

Shija amedai katika shtaka la kwanza, Rugaravu akiwa raia wa Rwanda, siku hiyo ya tukio, saa 4:00 asubuhi mshtakiwa alikutwa anaishi nchini bila kuwa na kibali.


Shitaka la pili, Rugaravu anadaiwa kughushi vibali vitatu vya makazi vyenye majina ya Winnie Bayisenge, Daoud Niyigena na Hasina Uwase kwa lengo la kuonyesha kuwa vimetolewa na Idara ya Uhamiaji, wakati akijua kuwa sio kweli.

Shitaka la tatu, linamkabili Munyakazi, anadaiwa kughushi kibali cha makazi chenye jina la Abduljalil Munyakazi kwa lengo la kuonyesha kuwa kimetolewa na Idara ya Uhamiaji, wakati akijua kuwa sio kweli.