Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dar wafurahia kasi Halotel ikiongoza ubora wa intaneti

Muktasari:

Wakati Vodacom, Airtel na Tigo zikinunua vitalu vipya vya intaneti ya 5G, bado Halotel imeendelea kuwa kinara wa kasi kubwa huku wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakielezwa kufurahia zaidi kasi nzuri  ya mitandao ya simu nchini.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiuza vitalu vitalu vya intaneti ya 5G hivi karibuni ili kuongeza kasi, ripoti inaonyesha kampuni ya Halotel ndio kinara huku wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakifurahia kasi zaidi.

 Licha ya Dar es Salaam, ripoti ya robo ya tatu mwaka huu ya Speedtest Global Index inayataja majiji mengine yanayopata kasi kubwa ya intaneti kuwa ni Mbeya, Arusha, Dodoma, Mwanza.
“Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanapata kasi ya Mb13.9 kwa sekunde wanapopakua kitu kutoka mtandaoni na kasi ya Mb8.75 wanapopakia kitu,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Mwanza linafuata kwa wakazi wake kupata kasi ya Mb13.45 kwa sekunde kupakua huku wakipakia kwa kasi ya Mb12.96 kwa sekunde.

Arusha wanapakua kwa kasi ya Mb11.29 kwa sekunde huku wakipakia kwa Mb7.77 na Mbeya ni Mb11.13 kwa sekunde kupakua na Mb6.44 kwa sekunde katika kupakua.

Wakati majiji hayo yakifurahia huduma, ripoti inasema wanaotumia mtandao wa Halotel wanapata kasi zaidi katika kupakia na kupakua.

Mtandao huo, ripoti inasema unampa mteja wake kasi ya Mb17.63 kwa sekunde anapopakua kitu huku ukifuatiwa na Vodacom yenye kasi ya Mb13.63 kwa sekunde.

Airtel inafuata ikiwa na kasi ya Mb11.61 kwa sekunde, Zantel na Tigo zikifuata zikiwa na kasi ya Mb6.01 kabla ya TTCL iliyo na kasi ya 5.12 kwa sekunde.

Wakati ripoti hii ikitoa ufafanuzi huo, tayari kampuni tano nchini zimeuziwa vitalu 11 ili kuimarisha kasi ya intaneti na kuwawezesha Watanzania kufurahia zaidi huduma za kidijitali.

Kwenye mnada uliofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivi karibuni, Vodacom na Airtel zilipata vitalu vinne kila moja, Tigo vitalu viwili na Halotel ikapata kimoja.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari alisema mnada huo umeiingizia Serikali jumla ya dola 187.496 milioni za Marekani (Sh436.2 bilioni).

“Kulikuwa na watoa huduma watano walishiriki kwenye mnada huo uliokuwa na vitalu 11 vya masafa, wanne wameshinda. Kampuni za Vodacom na Airtel zimepata vinne kila moja, Tigo imepata vitalu viwili na Halotel kimoja,” alisema mkurugenzi huyo.

Kwa vitalu hivyo, alisema Vodacom italipa dola 63.22 milioni sawa na Sh146 bilioni huku Airtel ikitoa dola 60.1 milioni sawa na Sh139 bilioni wakati Tigo ni dola 34 milioni na Halotel dola 30.16 milioni ambazo ni Sh69 bilioni.