Dawa za kulevya zamtoa machozi RC Makonda

Picha zikimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akilia huku ya kulia akibembelezwa na Mchungaji, Wilbroad Mastai aliposhiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kimara, jijini Dar es salaam jana. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Makonda ambaye alisali Misa ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara jana, alipewa nafasi ya kuzungumza.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alielezea  madhara ya dawa za kulevya na vita aliyoianzisha kiasi cha kumfanya abubujikwe machozi.

Makonda ambaye alisali Misa ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara jana, alipewa nafasi ya kuzungumza.

Aliitumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa vita hiyo, huku akieleza madhara ya dawa za kulevya kiasi cha kufikia hatua ya kulia na kukatisha hotuba yake.

Alisema vita hiyo si ya ulimwengu wa kimwili, bali ulimwengu wa Kiroho.

 

Wakati tukio hilo likitokea huko Kimara, Askofu Josephat Gwajima naye akiongoza ibada katika kanisa lake la Ufufuo na Uzima lililopo Ubungo, aliitumia fursa hiyo kuendeleza mashambulizi dhidi ya Makonda na mtu anayeitwa Daudi Albert Bashite.

Gwajima alituma ujumbe akisema yeye ni kama mashine ya kusaga na kukoboa na atakayemgusa atageuka kuwa sembe.

 

Wawili hao walijikuta katika mapambano baada ya Makonda kumtaja Askofu Gwajima katika orodha ya watu 65 waliotakiwa kuripoti kituo cha polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano kuhusu taarifa ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya na baadaye kiongozi huyo wa kidini alipimwa, kupekuliwa nyumbani na kukaa mbaroni kwa siku tatu kabla ya kuachiwa.

Baada ya kutoka, Askofu Gwajima alianzisha vita dhidi ya mkuu huyo wa mkoa, akimtaka aweke bayana vyeti vyake vya elimu huku akituhumu kuwapo dosari katika safari yake ya kielimu na wiki iliyopita aliitwa tena kituo cha polisi na kupekuliwa tena kabla ya kuachiwa.

 

Makonda alisema vita iliyopo ni kati ya mauti na uzima, kati ya haki na dhuluma na ni ya kuhakikisha mtoto wa mtu anatoka katika makucha fulani.

Alisema akimnukuu mchungaji wa kanisa hilo kuwa wasiumizwe na maneno ya watu kwa kuwa kazi wanayoifanya inalipa.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi