Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC aonya wafugaji kuwatandika viboko wakulima

Muktasari:

  • Migogoro ya wafugaji na wakulima yamwibua DC Same, aagiza kuundwa timu za usuluhishi za vijiji na kata.

Same. Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameziagiza halmashauri za vijiji na kata wilayani humo kuunda kamati za usuluhishi zitakazotatua  migogoro baina ya wakulima na wafugaji inayoendelea wilayani humo huku akionya wafugaji kuwachapa viboko wafugaji.

 Amesema kuwepo kwa kamati hizo zitapunguza kwa kiasi kikibwa migogoro hiyo huku akiwataka wakulima na wafugaji kuheshimiana na kwamba hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine.

Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo jana, wakati akisikiliza kero mbalimbali za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Ruvu wilayani humo ambapo kero kubwa ilikuwa ni migogoro ya wafugaji na wakulima iliyopo katika wilaya hiyo.

"Viongozi wa kata, vijiji, vitongoji hamuwajibiki ipasavyo, mngekuwa mnawajibika migogoro hii ya wafugaji na wakulima isingekuwepo kiasi hiki, mnatakiwa kuyamaliza huko lakini hamyamalizi na mnaileta kwa mkuu wa wilaya, wajibikeni viongozi wangu," amesema.

"Viongozi mkiwajibika kwenye maeneo yenu hii migogoro haiwezi kutokea, wakulima na wafugaji ni watu ambao wanategemeana, mkulima anamhitaji mfugaji na mfugaji anamhitaji mkulima, shida iko wapi ni kwa sababu ninyi hamheshimiani, mnaingiliana kwenye maeneo yenu," amesema.

Amesema zipo baadhi ya tabia za wafugaji kuwatandika viboko wakulima pale wanapotaka kuondoa mifugo inayoingia kwenye mashamba yao lakini wanaambulia viboko kitendo ambacho amesema hakikubaliki.

"Mkulima anapokwambia toa mifugo kwenye shamba langu wanatandikwa viboko, hii haikubaliki, naomba sana mheshimiane, naomba muishi kwa kuheshimiana, hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine hapa," amesema.

"Niwaagize viongozi wa serikali wa vijiji mliopo hapa, itisheni mikutano ya dharura undeni kamati zenye wakulima na wafugaji maana migogoro imekuwa mingi hapa, ili kunapotokea kwamba kuna kundi mojawapo limekiuka  taratibu zile kamati ziwe ndiyo kazi zake kusuluhisha migogoro," amesema.

Wakizungumza katika mkutano huo wa hadhara, wananchi wa vijiji vya Ruvu Marwa na Mferejini, wameeleza namna ambavyo wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye mashamba yao na wakati mwingine kupigwa na wafugaji hao pale ambapo wanafukuza mifugo isile mazao yao.

Ester Mnzava, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Ruvu Mferejini, amesema changamoto kubwa waliyonayo ni mifugo kuchungwa  kwenye mashamba yao wakati mazao yakiwa mashambani na kwamba wamekuwa wakipoteza muda mwingi  wakilinda mashamba yao yasivamiwe na mifugo.


"Mpaka sasa hivi nateseka na nimeshindwa hata kulipia watoto wangu shule, watoto wangu ni wadogo wanakufa njaa kwa ajili ya mifugo kula mazao yangu shambani, unakuta mtoto mdogo anaswaga mifugo kwenye shamba ukimfukuza unaambulia matusi na ukiangalia anayekutukana ni mtoto mdogo, inaumiza sana,"amesema mama huyo.

Peter Kaoneka ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ruvu Marwa, amesema ni wakati mwafaka sasa serikali kuja na suluhisho la kudumu la kutatua migogoro ambayo imekuwa ikiwagharimu Kila msimu wa mavuno.

"Tumekuwa walinzi wa mashamba siyo mchana wala usiku wenzetu wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye mashamba yetu na wakati mwingine mifugo kuharibu miundo mbinu ya maji ya mifereji ya maji, tunashindwa kuzalisha wakati mashamba tunayo, tunaomba serikali iwekeze nguvu kwenye kudhibiti halii maana ni mbaya wakati mwingine watu wamekuwa wakijeruhiana," amesisitiza.