Sheikh auawa ikidaiwa kupigwa na wafugaji

Viongozi mbalimbali wa dini pamoja na wananchi wakiswalia mwili wa Sheikh, Juma Omari aliyefariki dunia kwa kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji wilayani Handeni. Picha na Rajabu Athumani.
Muktasari:
- Sheikh Juma amefariki dunia ikidaiwa kupigwa na wafugaji ambao waliingiza ng’ombe shambani kwa shemeji yake, ambaye naye amejeruhiwa kichwani.
Handeni. Sheikh mmoja wa mji mdogo wa Mkata wilayani Handeni mkoani Tanga, Juma Omari inadaiwa kuuawa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji ambao waliingiza mifugo yao shambani.
Akisimulia mkasa huo baba mdogo wa marehemu, Hemedi Yahaya jana Jumapili Septemba 24, 2023 wakati wa mazishi amesema Sheikh Juma alikwenda shamba kumsaidia shemeji yake kufukuza ng'ombe walioingizwa na wafugaji na baadaye kutokea mapigano ambaye yalisababisha apate majeraha ambayo ni chanzo cha kifo.
Amesema, sheikh huyo alikwenda shambani kwa ajili ya kumsaidia shemeji yake ambaye wafugaji waliingiza ng'ombe shambani, ndipo kwenye shughuli ya kutoa mifugo hiyo yakaanza malumbano baina yao na wafugaji.
Amesema kuwa wafugaji hao walifika shambani na kuchukua mifugo yao na kubakiza ng'ombe mmoja na baadaye walirudi na kuanza kuwashambulia, ambapo shemeji yake marehemu amejeruhiwa kichwani.
"Marehemu Sheikh Juma alinipigia simu jana jioni kwamba anawenda shamba kumsaidia shemeji yake ambae amejeruhiwa, kuondoa ng'ombe waliokuwepo shambani na huko ndio walivamiwa na wafugaji wenye mifugo hiyo ambapo mmoja amejeruhiwa na huyu amefariki," amesema Hemedi.
Mwenyekiti Kamati ya Ulinzi Usalama na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo ametoa maagizo kwa viongozi wa vijiji, kata na tarafa kuwa kwa kupitia sherehe ndogo waanze kuchukua hatua.
Msando ameagiza kuwa kwa wafugaji waliopo Wilaya ya Handeni kinyume na utaratibu kuondoka mara moja na wafugaji wanaouza majani makavu shamba waache mara moja.
"Kutokana na sheria ndogo iliyotungwa kuanzia sasa ng'ombe watakaokamatwa ndani ya shamba lolote lile, hakuna kutozwa faini mhusika ila atataifishwa na serikali na siyo tena mali ya mhusika, hivyo viongozi wote wa ngazi ya kijiji na kata waanze kuifanyia kazi," amesema Msando.
Mwananchi wa Mkata, Bakari Kombo amewatupia lawama wasimamizi wa sheria ngazi ya vijiji, kata na tarafa kuwa kutochukua hatua kwao wananchi wanapotoa taarifa ndiyo sababu ya kuendelea matukio hayo.
Ameongeza kuwa serikali itilie mkazo suala la upimaji ardhi ili wananchi waweze kutambua, ni wapi ni eneo la wafugaji na wakulima ili kuweza kudhibiti matukio kama hayo.
Akiwa msibani hapo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Amiri Changongo amemtaka mkuu wa wilaya kufuatilia viongozi wa chini yake ambao wanatajwa kutowajibika kuchukua hatua.
Pia ametaka kufuatiliwa viongozi wa vijiji na kata ambao wametajwa kutochukua hatua, wanapopewa taarifa ya matukio ili hatua zaidi dhidi yao zichukuliwe na kukomesha matukio hayo.