DC Chunya azionya taasisi zinazolimbikiza madeni ya maji

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa maji wilaya ya Chunya wakati akifungua mkutano wa wadau. Picha Mary Mwaisenye 

Muktasari:

  • DC Mayeka pia ameshauri madiwani kuweka mikakati ya kulinda miundombinu ya maji ili kufanya miradi iwe endelevu na kuwaelimishe wananchi ili waone miradi hiyo iliyopo maeneo yao ya vijiji ni yao na wailinde ili kuepuka Serikali kuingia hasara.

Chunya. Mkuu wa wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Mayeka Mayeka amezitaka taasisi zilizolimbikiza madeni ya bili za maji kulipa mara moja ili kuepuka kukatiwa maji.

Mayeka ameyasema haya Oktoba 6, 2023 wakati akifungua mkutano wa nusu mwaka wa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii, (CBWSO's) kufuatia viongozi wa vijiji wa watumiaji kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo   ikiwepo ya taasisi kutolipa bili kwa wakati.

Wakati huo huo, Mayeka ameshauri madiwani kuweka mikakati ya kulinda miundombinu ya maji ili kufanya miradi iwe endelevu na kuwaelimishe wananchi ili waone miradi hiyo iliyopo maeneo yao ya vijiji ni yao na wailinde ili kuepuka Serikali kuingia hasara.

"Ni kweli Chunya kuna uhaba wa maji, lakini ikiwekwa mikakati mizuri hizi kero zitakwisha kwani uharibifu wa vyanzo na miundo mbinu unafanywa na wananchi wanaozunguka miradi hiyo kwani wakielimishwa vizuri miradi hiyo wataitunza kama wanavyotunza mali zao,” amesema Mayeka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri, Bosco Mwanginde akizungumza kwenye kikao hicho amewasa wasimamizi wa maji ngazi ya vijiji kuhakikisha wakuwa na lugha rafiki kwenye jamii ili kutengeneza mahusiano mazuri na wananchi ili miradi inayowekwa  na serikali  iweze kudumu.

Mwanginde amesema ushirikishwaji wa wananchi kwenye miradi iliyopo maeneo wanayoishi utasaidia kufanya miradi iwe endelevu na bora kutokana na wananchi kupata uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa miradi hiyo.

Awali meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) Wilaya ya Chunya, Ismail Ismail akizungumza katika mkutano huo, amesema wamejipanga kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama katia kata zote na kwamba wanunua magari ya kuchimba visima 26.

Naye Diwani Viti Maalumu, Fide Mwalukasa amepongeza Ruwasa kwanamna wanavyoendesha jumuiya hizo kwani kupitia jumuiya hizo wamesaidia kusogeza huduma kwa wanachi ukilinganisha na mwanzo.