DC Liwale awataka wakala wa vipimo kujikuta vijijini
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Liwale, amewataka Wakala wa Vipimo Mkoa wa Lindi (WMA), kujenga tabia ya kukagua mizani kila mara, hasa maeneo ya vijijini
Ruangwa. Mkuu wa wilaya ya Liwale, Goodluck Mlinga, amesema kuwa, Wakala wa Vipimo Mkoa wa Lindi (WMA), kujenga tabia ya kukagua, mizani mara kwa mara hasa maeneo ya vijijini, kwani kumekithiri udanganyifu wa vipimo.
Akizungumza, wakati alipotembelea banda la WMA, Mlinga amesema kuwa maeneo ya vijijini wananchi hawaelewi chochote, na kuwataka kuweka utaratibu wa kupima mizani kila wakati
"Wekeni utaratibu wa kutembelea vijijini kwani kule kuna changamoto kubwa sana, wauzaji wa mafuta kwenye vituo wanatabia ya kuwaibia mafuta wateja," amesema DC huyo na kuongeza;
"Jitahidini kwenda vijijni kwani wateja wengi wanaibiwa bidhaa zao kutokana na mizani kuwa nakasoro na wananchi wengi hawajui kama kuna taasisi kama yenu."
Aidha Meneja wa WMA Mkoa wa Lindi, Kessy Choka, amesema kuwa mara nyingi wanaweka utaratibu wa kuwatembelea iwe kwa kustukiza au kwa taarifa.
"Sisi kama Wakala wa vipimo, tuna utaratibu ambao tumeuweka wa kwenda kwenye vituo vya mafuta kwa taarifa na pia wakati mwingine tunashtukiza,” amesema Choka.
Kwa upande wake, Farida Sadiki, mkazi wa Ruangwa, amesema: “Kiukweli unaweza kwenda dukani wakati mwingine unapima unga kilo moja unaona tofauti kabisa unga ni mdogo sana jamani kama hao watu wapo wafike kwenye maduka labda wataacha kutuibia,” amesema Farida.