Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Mbulu aagiza wazazi wasiopeleka watoto shule wakamatwe

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara Chelestino Mofuga akikagua madaktari ya wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza wa shule ya sekondari Silaloda, kwenye ziara yake ya kutembelea shule zote 37 za sekondari za wilaya hiyo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Wazazi na walezi wilayani Mbulu mkoani Manyara ambao hawajawapeleka shule watoto wao wametakiwa kukamatwa.


Mbulu. Mkuu wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Chelestino Mofuga ameagiza wazazi wote na walezi ambao hadi sasa hawajawapeleka watoto wao shule za msingi walioandikishwa na waliofaulu sekondari, wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia, ameagiza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za sekondari ambao hawajaripoti wafanye hivyo mara moja ndani ya siku tatu.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo leo Jumatano Januari 30, 2019 kwenye ziara ya kukagua mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kwenye shule za sekondari akiwa na kamati ya ulinzi na usalama.

Amesema wazazi na walezi wa wanafunzi wote ambao watoto wao hawajafika mashuleni bila taarifa ya kueleweka wakamatwe na kulazwa mahabusu ili iwe funzo kwa wengine ambao hawajatimiza wajibu wao.

"Pamoja na hayo wanafunzi ambao hawajafika shuleni hadi sasa natoa siku tatu wote wasakwe waende shule wakasome ili kutimiza lengo la Rais John Magufuli la kutoa elimu bila malipo," amesema Mofuga.

Amesema Serikali imetimiza wajibu wake kwa kutoa elimu bila malipo, wazazi na walezi nao wanatakiwa wawajibike kwenye nafasi zao kwa kununua sare na mahitaji ya shule yanayohitajika.

Amewataka wakuu wa shule kuwasimamia walimu wao ipasavyo na kuwa na mpango mkakati wa kufaulisha wanafunzi badala ya kufundisha bila malengo kwani mwishoni wanafunzi wanashindwa kufaulu.

"Nimeagiza mkuu wa shule ya sekondari Silaloda kuandika barua ya maelezo na walimu wote na kuwasilisha wakiambatanisha nakala za vyeti vyao kwani ilikuwa na wanafunzi 11 na wote walifeli wakati walimu zaidi ya wanane ni wahitimu wa chuo kikuu," amesema.

Mmoja kati ya wanafunzi wa shule ya sekondari Singland, John Tsere amesema wanashukuru jitihada za ujenzi wa madarasa zinaendelea vizuri ili kuondokana na msongamano.

"Hivi sasa tunabanana kwenye madarasa ila mheshimiwa mkuu wa wilaya ametoa wiki mbili madarasa yamalizike ili tusome kwa kujinafasi na siyo kubanana tena," amesema Tsere.

Mofuga akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alikagua shule 10 za sekondari kati ya shule 37 za Mbulu zinazotarajiwa kukaguliwa na kamati hiyo.

Hadi mwishoni mwa mwaka jana wilaya hiyo ilikuwa na mapungufu ya vyumba 18 vya madarasa na sasa ina upungufu wa vyumba vinne pekee vya shule ya sekondari Singland.