DC Same amuonya mwekezaji shamba la mkonge
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akizungumza na wananchi wa kata ya Maore, wilayani humo(Hawako pichani) alipokwenda kutembelea eneo lenye mgogoro na kuzungumza na wananchi hao.
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amempa onyo mwekezaji wa shamba la mkonge la LM Investiment wilayani humo kwa kuzua uzushi kwamba wananchi wamevamia na kuchoma eneo lake.
Same. Mkuu wa wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amempa onyo mwekezaji wa shamba la mkonge la LM Investiment wilayani humo kwa kuzua uzushi kwamba wananchi wamevamia na kuchoma eneo lake.
Mkuu huyo wa wilaya amesema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Maore wilayani humo, akidai uwepo wa 'video clip' zinazosambazwa na mwekezaji huyo zikidai wananchi wamevamia eneo lake.
Mwaka 2018 serikali ilimega na kutoa eneo la ekari 300 kwa vijiji vitatu vya Ndugu, Msufini na Mpirani baada ya mwekezaji huyo kutelekeza eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 2000 kwa matumizi ya wananchi ambao walikuwa na uhaba ardhi.
"Mwekezaji huyu anachonganisha serikali na wananchi kwa kuchoma moto eneo lake mwenyewe na kudai kwamba wananchi wanahusika na kitendo hicho na kisha kupiga picha na kurusha 'video clip' kwenye mitandao ya kijamii,"amesema Mgeni.
Mgeni amesema alitembelea eneo hilo la mgogoro na kukagua mipaka na kubaini kuwa mwekezaji huyo, LM Investiment imekuwa ikisafisha na kuchoma majani kwenye eneo lake halali kisha kupiga picha na kuzirusha mitandao na kudai wananchi wamefanya uvamizi kwenye eneo lake jambo ambalo sio kweli.
"Baada ya kutembelea eneo hilo mimi na kamati yangu ya ulinzi tumebaini huyu mwekezaji amesema uongo lakini amezua taharuki kwa Watanzania na anataka kuonyesha kwamba Rais Samia Suluhu Hassan hajali wawekezaji kitu ambacho sio sahihi," amesema.
"Nitumie mkutano huu kumuonya mwekezaji dhidi ya vitendo vyake vya taharuki kwa kuwadanganya Watanzania kwamba wananchi wa hivi vijiji vitatu wanavamia maeneo yake na kuchoma mkonge, nampa onyo na atakaporudia tena serikali itamchukulia hatua za kisheria kwasababu anaichonganisha serikali na wananchi.
Akiongea kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa LM Investiment, Omari Mndeme amesema eneo lake hilo alinyang'anywa kinyume na utaratibu na kupewa wananchi hao na kwamba hayupo tayari kutoa eneo hilo.
"Kwanza tumenyanganywa eneo letu kinyume na sheria, alikuja William Lukuvi akiwa waziri mwaka 2018 akasema tutoe eneo ambalo halina mkonge lakini lilitolewa eneo ambalo lina mkonge na wakati eneo hilo linapimwa hatukushirikishwa kabisa, huwezi kuchukua eneo la mtu bila kumpa fidia," amesema.
"Sisi tunataka turudishiwe ardhi yetu maana hili eneo lilichukuliwa kwa nguvu hatuwezi kukubali kuachia mali zetu, hizo ekari 300 nitalipa na nini wakati nimechukua mkopo benki sinitafilisika, siko tayari na nimeandika barua kwa Rais kwa sababu hakuna barua iliyokuja kwa maandishi tukabidhi eneo," amesema.
Amesema eneo ambalo wananchi wamevamia na kuchoma moto ni eneo la mkonge lenye ukubwa wa ekari mbili na nusu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kata ya Maore,Rajabu Kijangwa na Yasin Hassan wamemshukuru mkuu wa wilaya hiyo kuingilia kati suala hilo ambalo limekuwa likiwanyima furaha kutokana na tabia ya mwekezaji huyo ambaye amekuwa akisafisha shamba lake kwa kuchoma nyasi kisha kurekodi video na kuisambaza mtandaoni huku akidai wananchi ndio wamevamiwa na kuchoma moto eneo lake jambo ambalo siyo la kweli.