DCEA yatahadharisha matumizi ya skanka kwa vijana

Bangi aina ya skanka ikiwe kwenye mifuko

Muktasari:

Skanka imebainika kuwa na kiwango kikubwa cha sumu na kemikali tofauti na iliyokuwa inatumika awali, huku madhara yake yakiwa ya haraka zaidi ikiwemo kusababisha matatizo ya akili yanayolazimisha kufanya uhalifu au kusababisha kifo.

Arusha. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),  imetoa tahadhari dhidi ya matumizi ya bangi mpya aina ya skanka,  kwa madai kwamba ina madhara ya haraka tofauti na nyinginezo.

Aina hiyo ya bangi iliyogundulika mwishoni mwa mwaka jana, imebainika kuwa na kiwango kikubwa cha kemikali tofauti na iliyokuwa inatumika awali huku madhara yake yakiwa ya haraka zaidi ikiwemo kusababisha matatizo ya akili yanayolazimisha kufanya uhalifu au kifo.

Tahadhari hiyo imetolewa leo Aprili 3, 2024 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alipokuwa akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.

Amesema, skanka ni bangi iliyoongezwa makali ya kemikali kwa usindikaji hadi kufikia asilimia 40 tofauti na bangi ya kawaida inayovunwa na kutumika yenye kiwango cha asilimia nane  hadi 15.

“Hii bangi imetokana na baadhi ya nchi zilizoruhusu kilimo chake kibiashara kukosa soko mwaka jana na kufikia hatua ya kusindika ili isiharibike, ndio ikasababisha kuongezeka kiwango cha kemikali, sasa wanaanza kuchepusha kutoka nchi zao kwenda nchi jirani ikiwemo Tanzania,” amesema Lyimo.

Ametaja baadhi ya nchi hizo zilizoruhusu kilimo cha bangi kuwa ni Uswatini, Afrika ya Kusini, Malawi na Zambia.

Bangi hiyo kwa mara ya kwanza ilianza kuingia nchini Agosti, mwaka jana kupitia mpaka wa Tunduma ambapo Lyimo amesema zilikamatwa zaidi ya kilo 75 ndani ya shehena za maboksi ya matunda aina ya tufaa (apple) iliyokuwa inaingizwa Tanzania kutoka Afrika Kusini.

“Hadi sasa tumeshakamata zaidi ya kilo 600 za skanka na watuhumiwa kesi zao ziko katika hatua tofauti tofauti, lengo ni kutokomeza kabisa biashara hii nchini Tanzania kutokana na madhara yake makubwa yanayojitokeza ikiwemo matukio ya ukatili,” amesema Lyimo.

Amesema moja ya madhara ya skanka ni kuleta ugonjwa wa afya akili (ukichaa) kwa haraka, lakini pia watumiaji wanakuwa wakatili mithili ya wanyama na kujikuta wakitaka kutekeleza matukio ya uhalifu ikiwemo ubakaji, ulawiti, uporaji, ujambazi, mauaji kwa kutumia vitu vyenye ncha kali, hivyo jamii inayowazunguka huathiriwa pia na kuwa hatarini.

“Kwa bahati mbaya vita hii imekuwa ngumu kidogo kwani wafanyabiashara wamekuwa wakitumia mbinu fiche sana ikiwemo kufungasha kama vitu halali kwenye nailoni na kuleta muonekano kama vitafunwa, karanga au majani ya Chai, hivyo tunaomba jamii itambue janga hili na watoe ushirikiano kutokomeza,” amesema Lyimo.

Akizungumza mjini Moshi, kwenye maadhimisho ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa jana, Aprili 2, 2024, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alieleza kusikitishwa na tabia ya vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na jinsi inavyowagueza vichaa.

“Hii bangi aina ya Skanka ina sumu nyingi na huchanganywa kwenye sigara lakini ukashaitumia, watumiaji wanabadilika na kuwa vichaa, ni wakati sasa vijana ambao mmekuwa mkitumia muache ili kunusuru maisha yenu kwani mtafanya Taifa hili kukosa Watanzania” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema waathirika wakubwa wa matumizi ya dawa hizo ni watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24.

Akizungumzia swala hilo, mkazi wa Arusha, Theresia Mitawas amesema dawa za kulevya zimekuwa janga kwa vijana na kuwafanya kuwa tegemezi, kutekeleza matukio ya ukatili lakini pia kukosa ustaarabu na heshima.

“Unakuta kijana mdogo wa miaka 18 au 20 hana nguvu hata za kujishughulisha na chochote kujiingiza kipato zaidi ya kushinda vijiweni mchana huku nyakati za usiku akipora watu au wakati mwingine kubaka na kulawiti watoto mitaani. Tunaomba Serikali iongeze nguvu kutokomeza madawa haya kwani ni janga kwa Taifa baadaye,” amesema Theresia.